Wabunge wamehoji masuala ya usambazaji wa gesi na umeme nchini

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu

Muktasari:

Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Azizi Mtamba  amehoji Serikali ina mpango gani wa kujenga chuo kitakachotoa mafunzo ya gesi na mafuta katika Kanda ya Kusini ili vijana wa mikoa hiyo na maeneo mengine waweze kupata taaluma na kushiriki kwenye sekta hiyo.

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Azizi Mtamba  amehoji Serikali ina mpango gani wa kujenga chuo kitakachotoa mafunzo ya gesi na mafuta katika Kanda ya Kusini ili vijana wa mikoa hiyo na maeneo mengine waweze kupata taaluma na kushiriki kwenye sekta hiyo.

Akiuliza swali hilo bungeni leo, Aziza amehoji kwanini Serikali haitaki kuwapa gesi kiwanda cha mbolea na lini itapeleka umeme katika maeneo ya mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara.

Akijibu, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kuvitumia vyuo vilivyopo nchini kuwajengea uwezo wa kitaaluma wananchi.

Amesema  mafunzi hayo yamekuwa yakitolewa katika masuala ya utafutaji, uendelezaji, uzalishaji, uchakataji, usafirishaji na mafuta na gesi asilia.

Subira amesema wapo wawekezaji waliingia mikataba na Halmashauri ya Mkindani ya kuwekeza kiwanda cha mbolea na gesi asilia.

Hata hivyo, amesema wawekezaji hao walitaka kuuziwa gesi hiyo kwa bei  ya chini ya ile iliyopangwa na Mamla ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).

Amesema mazungumzo yaliyofanyika baina ya Serikali na  wawekezaji hao pamoja na Kituo cha Uwekezaji (TIC) Machi mwaka huu wamefikia muafaka.

Amesema dhamira ya ujenzi wa kiwanda hicho ipo na kwamba kitawezesha wananchi wengi kupata ajira.

Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Fredina Kahigi  amehoji ni vigezo gani vilivyotumika kupeleka gesi ya bei nafuu Dar es Salaam badala ya Mtwara ambako gesi inaanzia.

Akijibu, Subira amesema waziri wa nishati  alizindua usambazaji gesi Mtwara  na kwamba viwanda 20  vimeunganishiwa na nishati hiyo katika jiji la Dar es Salaam.

Read more>> Upelelezi kesi ya Seth, Rugemalira haujakamilika