Wabunge waridhia kukatwa posho kumchangia mama wa pacha wanne

Mkazi wa Kinondoni, Radhia Solomon (wa pili kulia) aliyejifungua watoto wane Januari 8, 2019 akiwa na ndugu zake waliomsaidia kubeba watoto wake walipotembelea bunge jijini Dodoma leo. Wabunge wanawake watakatwa Sh50,000 na wanaume Sh100,000 kwa ajili ya kumsaidia Radhia. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Binti wa miaka 24, mkazi wa Magomeni Chemchem Jijini Dar es Salaam aliyejifungua watoto wanne leo Jumatatu Juni 3, 2019 ametembelea bungeni jijini Dodoma na wabunge kuridhia kumchangia fedha kwa ajili ya matunzo ya watoto hao.

Dodoma. Watoto ni baraka. Lakini unapopata watoto zaidi ya wawili ‘pacha’ changamoto huanza kuonekana katika malezi na namna ya kuwatunza kama ilivyotokea kwa Radhia Solomon (24).

Leo Jumatatu Juni 3, 2019 Radhia ametembelea bungeni jijini Dodoma na Spika Job Ndugai akatoa hoja kwa wabunge akitaka waridhie kukatwa posho zao za leo kwa ajili ya kumsaidia Radhia, hoja mbayo imekubaliwa na wawakilishi hao wa wananchi.

Licha ya hoja hiyo kuibua mvutano huku wabunge wakizungumza bila utaratibu, mwisho walikubaliana kuchangia Sh50,000 kwa wabunge wanawake na Sh100,000 kwa wanaume.

Aprili, 2019 Radhia alipewa talaka na muweke ikiwa ni siku 90 tangu ajifungue watoto hao. Alijifungua  pacha hao wanne Januari 8, 2019 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Spika Ndugai wakati anamtambulisha mwanamke huyo alianza kueleza jinsi anavyopitia katika wakati mgumu, hasa baada ya mumewe kumkimbia.

 “Haya baada ya kueleza haya nadhani tumchangie Radhia,” amesema Ndugai na kuwapa nafasi wabunge kueleza kiwango wanachopaswa kukatwa.

Pendekezo la mbunge wa Viti Maaum (Chadema), Susan Lyimo kutaka wabunge wanawake kukatwa kiasi hicho na wanaume  Sh100,000 ilipitishwa na Ndugai licha ya baadhi ya wabunge kusikika wakipinga akiwemo mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy.

Watoto wa Radhia  wa kike ni wawili Faudhia na Fardhia  na wa kiume wawili Suleiman na Aiman ni pacha ambao kila mmoja alikuwa na mfuko wake wa uzazi.

Soma zaidi: