Wabunge watofautiana kauli ya DPP

Muktasari:

Siku moja baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga kusema kuna baadhi ya wabunge wanapenyezewa rushwa na watu wanaokabiliwa na mashtaka au tuhuma mbalimbali za makosa ya jinai, ili wamshinikize katika utendaji wake, baadhi ya wabunge jana wamefunguka.


Dodoma. Siku moja baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga kusema kuna baadhi ya wabunge wanapenyezewa rushwa na watu wanaokabiliwa na mashtaka au tuhuma mbalimbali za makosa ya jinai, ili wamshinikize katika utendaji wake, baadhi ya wabunge jana wamefunguka.

DPP Mganga aliibua tuhuma hizo wakati akijibu tuhuma zilizotolewa na wabunge wawili wa upinzani, akiwamo Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), kwamba amekuwa akiwabambikizia watu kesi za utakatishaji fedha na kukubaliana nao walipe faini, kama chanzo cha kuongeza mapato ya Serikali.

Akizungumza jana na Mwananchi jijini Dodoma, Mbunge wa Mbozi (Chadema), Paschal Haonga alisema: “Hii ni tuhuma nzito, DPP hapaswi kufanya siasa, alichokifanya ameshambulia muhimili na anapaswa kuitwa hata katika Kamati ya Maadili (ya Bunge) ili aje awataje hao wabunge.

“Hili Bunge lina zaidi ya wabunge 360, sasa kusema baadhi yao wanapewa rushwa ni jambo zito na si dogo hata kidogo, DPP aje kwenye kamati na awataje hao kuwa ni fulani na fulani lakini kuishia kusema baadhi, haikubaliki,” alisema Haonga.

Mbunge wa Serengeti (CCM), Chacha Marwa alisema, “inawezekana kukawepo na vitendo hivyo kwa sababu mbunge ni nani? Mbunge si malaika, mbunge si Mungu, mbunge ni binadamu ambaye anaweza kufanya jambo lolote.”

Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka alisema kauli ya DPP haiwezi kuwa ya kukurupuka, bali atakuwa ameifanyia utafiti mkubwa na kuuridhisha.

Profesa Tibaijuka alishauri DPP badala ya kuzungumza nje, ashughulike na hao wabunge kwa sababu uwezo huo anao.

“Mimi ninachoweza kusema ni ule msimamo wangu niliochangia hata bungeni kwamba, kuna baadhi ya sheria hazijakaa sawa ndiyo maana tunaonekana kama kusimama kwa watuhumiwa,” alisema Tibaijuka.

Alisema msimamo wake aliutoa ndani ya Bunge kwamba suala la kuwaweka ndani watuhumiwa kwa muda mrefu halafu mwisho anaambiwa hana hatia, si jambo jema badala yake kama uchunguzi bado basi wawe nje.

Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko alisema hana sababu za kupinga kauli ya DPP kwani kila mtu na mtazamo wake. Matiko alisema DPP naye anatakiwa kuangalia kwani kuna vitu wabunge wanazungumza ukweli hivyo asichukulie wamehongwa.

Alitolea mfano kila kosa sasa limekuwa ni uhujumu uchumi halafu faini zinazotozwa haijulikani zinaingia mfuko upi na matumizi yake ni yepi.

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alisema anatafuta ukweli wa kauli hiyo na akijua atakuwa na nafasi nzuri kumjibu.