Wabunge watofautiana mjadala wa uhuru wa vyombo vya habari nchini

Dodoma. Wakati kesho mjadala wa bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ukitarajiwa kuendelea bungeni jijini Dodoma, baadhi ya wabunge wameeleza sababu za Tanzania kushuka kwenye viwango vya uhuru wa habari.

Tanzania imeshuka kutoka nafasi ya 93 mwaka jana hadi nafasi ya 118 kati ya nchi 180 duniani kwa mwaka huu kwa mujibu wa ripoti ya 2019 ya World Press Freedom Index.

Mjadala wa bajeti hiyo ya mwaka 2019/2020 ulianza Alhamisi iliyopita kwa wabunge takribani saba kuchangia, huku wanne wa upinzani wakizungumzia kuporomoka kwa uhuru wa vyombo vya habari.

Wakati wabunge wa upinzani waliozungumza na Mwananchi wakitoa maoni yao, wenzao sita wa CCM walikataa kuzungumzia jambo hilo, akiwamo wa Chemba, Juma Nkamia aliyesema anukuliwe kuwa amesema hana cha kuzungumza.

Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini ameeleza sababu kadhaa za Tanzania kushuka kwenye viwango hivyo kuwa ni pamoja na kuminywa kwa baadhi ya vyombo vya habari, kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara, watu kutokuwa na uhuru wa kujieleza na kutoonyeshwa kwa vikao vya Bunge.

Kaimu mnadhimu huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema, “Katiba iheshimiwe kwa sababu ndani ya Katiba tumepewa uhuru wa kutoa na kupokea habari. Hilo halipo kwa sasa, vyombo vingi vya habari vimedhibitiwa.”

Selasini alisema hata hotuba za kambi hiyo bungeni kuhusu wizara mbalimbali zinaondolewa baadhi ya maneno.

“Hivi sasa hata mtu akiitisha mkutano na wanahabari, vyombo vya habari baadhi huzuiwa kutumia habari hiyo. Nadhani hapa hoja si kupambana na vyombo hivi, wapambane na mtoa habari,” alisema Selasini.

Mbunge huyo wa Rombo alisema ndiyo maana mwaka huu taarifa za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zilikuwa na ‘madudu’ mengi kwa sababu ya kuwaminya watu katika maeneo mbalimbali nchini.

Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alisema hali ya uhuru wa habari hairidhishi.

Mbunge wa Liwale (CUF), Vedasto Ngombale alisema, “Unaposema uhuru wa vyombo vya habari unazungumzia mambo mengi, mfano urushwaji wa vipindi vya televisheni, Bunge Live. Mfano hivi sasa televisheni nyingi hazionekani.”

“Uhuru wa watu kutoa mawazo yao ni shida, mikutano ya hadhara nayo imezuiwa. Kushuka kwa nchi yetu katika suala hilo si jambo la kushangaza kwa sasa,” alisema Ngombale.

Katika mjadala wa bajeti hiyo wabunge wa upinzani walitolea mfano kufungiwa kwa magazeti, sheria kandamizi za habari, kuzuiwa kwa vikao vya Bunge kuonyeshwa moja kwa moja pamoja na uwepo wa magazeti yanayoandika habari za kuchafua watu lakini hayachukuliwa hatua huku mengine yakionywa na hata kufungiwa.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ambaye pia ni msemaji mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas alinukuliwa na Mwananchi Aprili 20, 2019 akisema Serikali inajua inachokifanya kwa Taifa.

“Kwanza kama Serikali hatujashangazwa na ripoti hiyo kwa sababu tunajua nini tunakifanya kwa faida ya Tanzania ya leo na kesho.”

“Huwezi kupima uhuru wa habari kwa kuorodhesha matukio ambayo yanajitokeza katika jamii na siyo yanayotendwa na Serikali kama la Azory (Gwanda),” alisema Dk Abbas na kuongeza.

“Huwezi kupima uhuru wa habari eti kwa kuangalia kuna waandishi wa CPJ walikuja Tanzania licha ya kukiuka sheria na taratibu za nchi wanapokamatwa unasema unakiuka uhuru wa habari.”

“Hili tutalifanya bila kujali ripoti gani ina mtazamo gani kwetu, kwetu sisi tuna jukumu la kikatiba kufanya hivyo.