Wachimba madini waandamana kumpongeza Magufuli, Mnyeti atoa neno

Viongozi wa wachimbaji wa madini ya Tanzanite na wanunuzi wakiwa kwenye maandamano ya kumpongeza Rais John Magufuli kupunguza tozo na kodi mbalimbali kwenye sekta ya madini nchini kwenye mji wa Mirerani wilaya ya Simanjiro mkoa wa Manyara leo.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewataka wachimbaji madini ya Tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro kuacha kutoa taarifa potofu za wizi wa madini aliodai kuwa haupo

Mirerani. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewataka wachimbaji madini ya Tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro kuacha kutoa taarifa potofu za wizi wa madini aliodai kuwa haupo.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Februari 16, 2019 wakati akipokea maandamano ya wachimbaji madini wa Mkoa wa Manyara waliolenga kumpongeza Rais John Magufuli kwa kuwajali.

Amesema baadhi ya wachimbaji na wananchi wa eneo hilo wamekuwa na mtindo wa kutoa taarifa potofu na wanapotakiwa kudhibitisha wanashindwa.

"Hivi karibuni kuna jamaa mmoja ametoa taarifa kuwa eti madini yameibiwa na kwamba ametoa taarifa kwangu sijafuatilia, si kweli maana hata ofisini kwangu sijamuona," amesema Mnyeti.

Amesema kati ya maeneo ambayo yanazungumza mambo ya uongo ni Mirerani kutokana na kutoa taarifa ambazo hazina uhakika.

"Eti anasema anataka kumuona Rais Magufuli na kumueleza wizi unaofanyika. Ofisini kwangu kwangu  hajafika na hata ningekutana naye angetaka nimtafutie kazi kwenye makampuni," amesema Mnyeti.

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (Marema),  Justin Nyari amesema wamefanya maandamano hayo ili kumpongeza Rais Magufuli kwa kuwaondolea kero wachimbaji madini wa eneo hilo na Tanzania kwa ujumla.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula amesema Rais Magufuli amewaheshimu wachimbaji hivyo nao wamuheshimu kwa kulipa kodi.

Chaula amesema wachimbaji wamepunguziwa asilimia zaidi ya 25 ya kodi hivyo walipe kodi hizo kwa maendeleo ya nchi.