Wachimbaji wa madini ya Ruby waandamana kudai mishahara yao

Wachimbaji wa madini ya Ruby Kijiji cha Kitwai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiandamana kwenda ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo kwa lengo la kudai stahili zao kwa mwajiri wao. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Wachimbaji wa madini ya Ruby Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, waandamana hadi kwa mkuu wa wilaya wakiomba Serikali kuingilia kati ili walipwe malimbikizo ya mishahara yao.

Simanjiro. Wachimbaji 35 wa mgodi unaomilikiwa na Raphael Mollel wa madini ya Ruby kijiji cha Kitwai, wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wameandamana hadi ofisi za mkuu wa wilaya hiyo wakiomba Serikali kuingilia kati ili walipwe malimbikizo ya mishahara yao ya mwaka mmoja.

Maandamano hayo yalifanyika jana jioni Ijumaa Januari 18, 2019 kuanzia mgodi wa Ruby hadi ofisi za mkuu wa wilaya umbali wa takriban kilomita 20.

Mmoja kati ya wachimbaji hao, Msafiri Waziri amesema wanadai fedha zao za zaidi ya mwaka na wakimuomba mmiliki awalipe anawazungusha.

Waziri amesema Serikali imeshachukua kodi na mrabaha kutoka kwa mmiliki wa mgodi huo baada ya kuzalisha madini hayo, lakini wao hawajalipwa stahiki zao.

Mchimbaji mwingine, Lembris Abraham ameiomba Serikali iingilie kati kwani wamefanya kazi kwenye mgodi huo muda mrefu.

"Tunadai fedha zetu za asilimia 10 ya madini yatakayopatikana lakini hatujalipwa ilhali tuna familia zinazotutegemea, tutaishije sasa?" amehoji Abraham.

Mkuu wa wilaya hiyo, Zephania Chaula amesema baada ya kukutana na wachimbaji hao na mmiliki wa mgodi huo amewapa siku saba ili wakutane kutatua mgogoro wao.

"Baada ya wachimbaji hawa kufika ofisini kwangu  tayari nimemuita na kuzungumza naye  mmiliki wa mgodi ili amalize mgogoro huu, lakini kwa ushirikishwaji na uwazi uwepo ikiwamo utekelezaji wa mkataba wao wa kupatiwa asilimia 10 ya uzalishaji baada ya makato ya matumizi," amesema na kuongeza:

"Nimemshauri mwenye mgodi kuwa na utaratibu wa kukutana na wachimbaji wake mara moja kila wiki ili asikilize changamoto na ushauri wao kwani wao ni familia moja."

Naye mmiliki wa mgodi huo, Raphael Mollel amethibitisha kuwapo kwa mgogoro huo na  kueleza kuwa wachimbaji  walikuwa na mkataba wa kazi lakini baadhi walidai hawajui kusoma wala kuandika.

"Nitalifanyia kazi agizo la mkuu wa wilaya tupate mwafaka kisha turudi kwake kwa ajili ya kumpa mrejesho juu ya mustakabali wa jambo hilo,” amesema.