Wadau wataka Kiswahili kiuzwe duniani kama bidhaa

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (kulia) akimkabidhi cheti cha ushiriki mmoja wa washiriki wa kongamano la Kiswahili la kimataifa lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (Bakiza). Picha na Haji Mtumwa

Hivi karibuni Zanzibar ilibahatika kuwa mwenyeji wa makongamano makubwa mawili ya kimataifa ya lugha ya Kiswahili, ambayo yaliwakutanisha wataalamu waliobobea kwenye lugha hiyo kutoka Afrika Mashariki, Marekani, Ujerumani, Misri na maeneo mengine.

Kongamano la kwanza lilifanyika Desemba katika ukumbi wa Shekh Idrissa Abdulwakili, Kikwajuni mjini Unguja, ambalo liliandaliwa na Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza) na kuhudhuriwa na washiriki zaidi 200 kutoka ndani na nje ya nchini.

Kongamano la pili liliandaliwa na Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (Chaukidu) na kufanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza) kampasi ya Vuga mjini Unguja ambapo zaidi ya washiriki 150 walihudhuria.

Makongamano yote hayo yalikuwa na lengo la kuitangaza lugha ya Kiswahili, ambayo hivi sasa inaonekana kuwa ni sehemu ya soko la biashara kama zilivyo bidhaa nyingine.

Malengo mengine ya makongamano hayo yalikuwa ni kuweka bayana matumizi mabaya ya lugha ya Kiswahili hasa kwa vijana ambao wanaonekana kuwa nyuma katika matumizi bora ya lugha hiyo adhimu duniani kote.

Katika makongamano hayo viongozi na washiriki walipata nafasi ya kutoa michango yao katika kuhakikisha Kiswahili kinaendelea kutumika kama sehemu ya biashara, pia inatunzwa vyema bila ya kupotoshwa.

Miongoni mwa viongozi ambao walipata nafasi ya kutoa michango katika makongamano hayo alikuwa ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hasaan ambaye alipata nafasi hiyo wakati akifungua kongamano lililoandaliwa na Chaukidu na kufanyika Vuga.

Samia alisema Kiswahili sasa ni sehemu ya bidhaa ya kibiashara, hivyo ni vyema kwa jamii kubadili fikra kwa kuchunguza na kufikiria jinsi ya kutumia vipengele mbalimbali vya lugha hiyo na utamaduni wake kama inavyotakiwa.

“Sote ni mashahidi wa namna Kiswahili kinavyoendelea kukua kwa kasi na kuwa si lugha tu bali ni bidhaa yenye tija katika soko la utandawazi, hivyo nasi tuna wajibu wa kubadili fikra zetu katika bidhaa yetu hii,” alisema Samia.

Samia alifahamisha kuwa, ushahidi uko wazi kwamba Kiswahili kimepiga hatua kubwa nje ya Tanzania na Afrika Mashariki na kwamba ni miongoni mwa lugha tatu za Kiafrika zenye wazungumzaji wengi zaidi ikishindana na lugha za Kihausa na Kiarabu.

“Hatua hii iliyofikiwa na lugha yetu ya Kiswahli ni ya kujivunia na hapa nitoe wito kwenu nyote kutumia fursa zilizopo ndani na nje kwa kukichukulia Kiswahili kama bidhaa muhimu kwa maendeleo yetu, kudumisha umoja, mila, tamaduni na desturi zetu,” alisisitiza.

Samia alikosoa tabia iliyoanza kushamiri hivi sasa ya kupotosha baadhi ya maneno ya Kiswahili hasa katika vyombo va habari, akiitaka Chaukidu na vyama vyengine kusimama imara kwa kuwarudisha kwenye mstari wanaoiharibu lugha hiyo ama kwa makusudi au kwa kutojua.

Samia pia alikipongeza Chaukidu kwa kuhakikisha Kiswahili hakimezwi na lugha za kigeni na kukifanya kiendelee kuota mizizi kwa kusambaa maeneo mbalimbali duniani.

Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akifungua kongamano lililoandaliwa na Bakiza alisema Kiswahili kinapaswa kuendelezwa na kutumiwa kwa fahari hasa ikizingatiwa ukubwa wa thamani yake katika mataifa mbalimbali duniani.

Alisema lugha ni sehemu ya utamaduni, hivyo jitihada za kukiendeleza na kukihifadhi Kiswahili zinapaswa kuchukuliwa na kila mmoja ili kuona lugha hiyo inaendelea kuzitangaza nchi husika na kuziingizia mapato.

Dk Shein aliweka bayana ukubwa wa Kiswahili kwa kusema kina watumiaji ambapo zaidi ya vyuo vikuu 100 duniani vinaifundisha lugha hiyo na zaidi ya vituo vya redio 100 vikiwemo vya Uingereza, Marekani, Ujerumani, China, Japan na Ufaransa vinatangaza kwa lugha ya Kiswahili.

Mtaalamu wa Kiswahili kutoka Kenya, Wala bin Walad alitaka Zanzibar ipewe heshima yake kwa kuwa ndio chemchem ya Kiswahili kitamu na fasaha ukilinganisha na nchi mbalimbali ndani ya Afrika na Ulaya. Walad alikiri kuwa Kiswahili nchini Kenya kimepiga hatua kubwa kwa kutumia vitabu vya waandishi wa Zanzibar.