Wadau wapendekeza namna ya kupunguza matumizi ya mkaa

Muktasari:

  • Ushauri wa wadau hao umetokana na Jukwaa la Fikra lililofanywa na Kampuni ya Mwananchi Communications, likihusisha watalaamu, wananchi na wanataaluma mbalimbali jijini Dar es Salaam

 

Dar es Salaam. Serikali imesema haitapiga marufuku biashara ya mkaa kwa sasa, lakini imeona haja ya kuratibu vizuri zaidi matumizi nishati hiyo baada ya wadau kujadili umuhimu na athari zake kimazingira na kutoa mapendekezo kadhaa.

Biashara ya mkaa kurasimishwa na kuwekewa kodi, bei ya umeme kushushwa, matumizi ya gesi asili, kutafutwa kwa teknolojia itakayowezesha miti kutumika kwa ufanisi kuchoma mkaa na kupiga marufuku majiko yasiyowekewa udongo pembeni ni miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na wadau wakati wa Jukwaa la Fikra la Mwananchi juzi usiku.

Jukwaa hilo, linalokutanisha viongozi wa Serikali, taasisi, kampuni, wadau wa masuala mbalimbali na wananchi kutafuta suluhisho la pamoja, lilifanyika kwenye ukumbi wa Kisenga uliopo jengo la Millenium Towers. Liliandaliwa kwa pamoja na Mwananchi Communications (MCL)na ITV/Radio One.

Juzi usiku wakati wa mjadala huo wa tatu tangu kuanzishwa kwa jukwaa hilo, wadau walijadili mada ya Mkaa, Uchumi na Mazingira Yetu ambako Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), January Makamba alisema Serikali imenufaika nao na kuahidi kufanyia kazi mapendekezo kwa kuanzia na kuunda timu itakayojadili masuala hayo.

Miongoni mwa wadau watakaokaa pamoja ni Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Nishati na wadau wa mazingira ikiwamo Ofisi ya Rais Muungano na Mazingira.

“Suala la uratibu wa shughuli za mkaa, Waziri Mkuu ameona na ametafuta namna bora ya kutuita tukutane kwenye mwamvuli mmoja kwa ajili ya kupata suluhisho,” alisema. Makamba alisema suala la kurasimishwa biashara ya mkaa ili iweze kuthaminishwa, linafanyiwa kazi pamoja na suala la sera ya tungomotaka inayohusisha mkaa na kuni likiwa chini ya Wizara ya Nishati.

“Niliwahi kuandika barua kwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo akiwa Profesa Sospeter Muhongo kuomba tuharakishe hatua ya kuandika sera ya tungomotaka nikitaka iwe sera tofauti kabisa, isiwe ndani ya nishati,” alisema Makamba.

“Mimi kama waziri mwenye dhamana ya mazingira naona ni ukweli kukata miti kunaathiri mazingira. Tutapambana na mambo hayo, ni wazi kuwa kuna gharama kubwa na kuongezeka umaskini kwa kukata miti. Kunaweza kuwa na lugha mbalimbali lakini ukweli ni kwamba kunaathiri mazingira.

“Bado nataka nishawishike kuwa unaweza kutengeneza utaratibu ukavuna miti uliyoipanda ukauza na bado ukapambana na mkaa mwingine wa kawaida, ” alisema Makamba.

Alisema nchi inayoongoza kwa kununua mkaa ni Ujerumani ikiwa ni asilimia 80 ya mkaa wote unaouzwa duniani na Tanzania ikiwa ni namba nne kwa kuuuza nje. Hata hivyo, alisema Ujerumani wana miti na hawachomi mkaa.

Inawezekana katika hili unatumika mgongo wa wanyonge, lakini wanaonufaika ni wauzaji wakubwa. Alisema asilimia 54 ya bei inakwenda kwa msafirishaji na kumuacha mnyonge anayechoma mkaa akiwa maskini, hana nyumba ya bati na hajaboresha maisha yake. Alisema kuondokana na mkaa ni safari na hakuna atakayeweza kuufungia kwa sasa, lazima safari hiyo ianze na inapaswa iendane na uvumbuzi.

“Gharama itapunguzwa kwa teknolojia na ubunifu. Kuna nafasi kubwa ya sekta binafsi ya kufanya hii biashara, hata washirika wa maendeleo wana nafasi hiyo pia,” alisema.

Mmoja wa wazungumzaji wanne wakuu katika jukwaa hilo, Ali Mufuruki ambaye ni mfanyabiashara maarufu na mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira, alisema suluhisho la tatizo la mkaa ni wananchi kuelewa.

Alisema licha ya umeme kuonekana ni nishati muhimu, ni asilimia mbili tu ndiyo inatumika licha ya kupatikana nchi nzima.

Alisema asilimia 92 ya nishati inayotumika nchini inatokana na mkaa na kuni. Alisema teknolojia ya umeme jua iligundulika miaka 70 iliyopita, lakini haijaweza kutumika kwa ufanisi kwa sababu ya uwepo wa mafuta na haikuwa ikipatikana kwa urahisi maeneo mengi, gharama zake kuwa kubwa.

Alisema ni ukweli ulio dhahiri kuwa kila mmoja ni mdau wa mkaa kwa sasa.

Alisema biashara na matumizi ya mkaa na kuni ni dola 75 bilioni za Marekani wakati Pato la Taifa (GDP) ni dola 50 bilioni.

Alisema ndio maana ni vigumu kuiondoa biashara hiyo kwa sababu ina nguvu kiuchumi na wala si kwa ajili ya kuwanufaisha maskini kama inavyodaiwa.

Alisema nchi zilizoendelea zilifanikiwa kuuondoa kwa kuweka kodi kubwa, kutoa vishawishi kwa watu kutumia nishati mbadala na kupunguza bei.

Rose Salingwa, mmoja ya wachangiaji kwenye mada hiyo, alisema miti ya asili ndiyo inayotoa mkaa mzuri hivyo itafutwe njia mbadala ya kuendeleza miti asili kwa sababu mkaa utokanao na miti ya kupandwa haupendwi.

Charles Meshack, mkurugenzi mtendaji wa TFCG, alisema kuna namna ya kufanya mkaa kuwa endelevu, akipendekeza kuwapo kwa utaratibu wa kukata miti kitaalamu ili ichipue tena na kukatwa baada ya miaka 18 hadi 24.

Mchangiaji mwingine, Marwa Samwel ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema suluhisho la mkaa lisiangaliwe kama linatoa ajira na mapato, bali lichukuliwe kama janga la kitaifa ili kila mtu aogope kukata miti.

Edward Maduhu ambaye ni mfanyabiashara na mtafiti wa misitu, alisema suluhisho la kupunguza uharibifu wa mazingira si mkaa peke yake, bali na mbao, hivyo suluhisho ni kujenga viwanda vya mkaa mbadala.

Alisema Tanzania inatumia mbao asilimia 35 na inayobaki inatupwa, ikitumika yote kwa asilimia 100 hiyo iliyobaki na kutupwa ndiyo inatengeneza mkaa.

“Hapa nchini wameachiwa maskini ndiyo wanafanya hiyo kazi ya kutengeneza mkaa, ndiyo maana madhara yanakuwa makubwa zaidi,” alisema.

“Njia pekee ya kudhibiti ni kuweka kodi kwenye bidhaa hiyo hivyo kutakuwa na usawa sokoni kati ya mkaa halisia na mkaa mbadala.”

Mchangiaji mwingine, Dk Donati Ulomi alisema Serikali ihakikishe inawajengea vijana uwezo wa jinsi ya kuzalisha mkaa mbadala na hakuna haja ya kuogopa mkaa wa kawaida kwa kuwa utapotea.

“Serikali ifungue soko la mkaa mbadala na iwekeze kwa kutangaza kuwepo kwa nishati mbadala ili watu wengi waitumie, pia kuweka eneo maalumu la kuuzia bidhaa hizo. Hiyo itasaidia kuzalisha ajira, kuongeza kipato kwa watengenezaji na kunusuru mazingira,” alisema Dk Ulomi.

Akichangia mada hiyo, mkurugenzi wa kampuni ya Mkaa Endelevu inayojishughulisha na utengenezaji wa mkaa mbadala, Benjamin Lane alisema nishati zipo kwenye utaratibu maalumu.

Alisema mkaa ukiwekewa utaratibu wa namna ya kulipa kodi, bei itapanda na watumiaji watahama na kutumia njia mbadala.

“Kwanza kuzuia uingizaji na kukuza nishati mbadala, kuzalisha mkaa mbadala na uwekezaji na mkaa uendelee kutumika na TRA wakusanye fedha kupitia nishati hiyo. Biashara itapanda na kutakuwa na ushindani wa matumizi ya mkaa na nishati nyingine,” alisema.