Waethiopia waja kujifunza utunzaji wa misitu Tanzania

Mkurugenzi wa Kituo cha Utafititi cha Central Ethiopia EV+& Forest Wondnossen Tsadik akizungumza wakati wa kikao cha majadiliano kati yao na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)

Muktasari:

Waethiopia wameguswa na namna rasilimali hiyo inavyolindwa na kupewa kipaumbele tofauti na ilivyo katika nchi yao. Wataalamu hao wametoka katika taasisi mbalimbali zinazohusika na utunzaji misitu na tafiti wametembelea mikoa ya Tanga, Morogoro, Iringa na Dar es Salaam.

Wataalam kutoka taasisi zinazojihusisha na misitu nchini Ethiopia wameipongeza Tanzania kwa hatua inazochukua kulinda misitu na kuhakikisha rasilimali hiyo inatunzwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Watalaamu hao 15 walikuja nchini kwa ziara ya kikazi lengo likiwa ni kujifunza namna bora ya utunzaji misitu kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Taarifa iliyotolewa na TFS leo Machi 17, 2019 imeeleza kuwa wataalam hao wametoka katika taasisi mbalimbali zinazohusika na utunzaji misitu na tafiti na  wametembelea mikoa ya Tanga, Morogoro, Iringa na Dar es Salaam.

Wageni hao wameeleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zina utaratibu mzuri wa usimamizi wa misitu.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti cha Central Ethiopia EV+ & Forest, Wondnossen Tsadik amesema kikubwa ambacho wamejifunza ni namna sekta ya misitu inavyoangaliwa kwa ukaribu zaidi.

"Tumeona hapa misitu inasimamiwa na TFS  ambayo iko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, hii inafanya kuwepo na ukaribu wa kufuatilia hatua kwa hatua kuhusu uhifadhi. Kwetu sisi mambo ya misitu yamechanganywa na mambo ya kilimo. Tunaipongeza Tanzania kwa namna ambavyo inasimamia misitu yake," amesema.

Pia amesema wakiwa katika maeneo mbalimbali ambayo wamekwenda wamepata nafasi ya kukutana na watalaam wa masuala ya misitu pamoja na watafiti wa kada mbalimbali na kubadilishana uzoefu.

Kwa upande wake Meneja wa Rasilimali za Misitu wa TFS, Dk Masota Abel amesema Waethiopia hao wameichagua Tanzania kwa sababu inasifika kwa utunzaji mazingira na hivyo ni muhimu kwa Watanzania wakaliona hilo na kuendelea kutunza rasilimali hiyo.

“Wageni wetu wamekiri na kukubali kazi nzuri inayofanywa na Serikali yetu kupitia TFS katika kutunza misitu, wameeleza namna kile ambacho wamejifunza watakavyokwenda kwao kuweka mikakati itakayowawezesha kuitunza misitu yao. Ethiopa misitu yao imeendelea kuharibiwa. Tunaweza kusema hawana misitu tena. Kwao eneo kubwa limebaki kuwa jangwa,”

Dk Abel ametumia fursa hiyo kuwashauri kuja kuwekeza Tanzania hasa katika sekta ya misitu na viwanda.