Wafanyabiashara wakubali kulipia maduka waliyoyajenga

Muktasari:

  • Mvutano kati ya halmashauri yawilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza  na wamiliki wa vibanda 98 vya maduka yanayozunguka Soko Kuu la Nansio wilayani humo juu ya nani mmiliki wake imefikia tamati baada ya wafanyabiashara kuridhia kuviacha na kuwa wapangaji.

Ukerewe. Mvutano wa zaidi ya miaka 12 kati ya halmashauri ya wilaya Ukerewe na wamiliki wa vibanda vya maduka yanayozunguka soko kuu la Nansio umekwisha baada wamiliki hao kukubali viwe mali ya halmashauri hiyo.

Vibanda hivyo 98 vilivyojengwa na watu binafsi kati ya mwaka 1991 na 1998 kwa kupata vibali vya halmashauri na kuendelea kuwa mali yao hadi sasa.

Pande hizo mbili zilijikuta zinaingia kwenye mvutano huo mwaka 2007 baada ya halmashauri kuibuka na kudai umiliki wao wa miaka 10 ulishafika kikomo, hivyo vibanda hivyo ni mali ya halmashauri ya Ukerewe.

Tangu wakati huo, zaidi ya miaka 12 iliyopita, kumefanyika vikao kati ya pande hizo mbili lakini mwafaka haukupatikana.

Makubaliano hayo yamefikiwa Januari 12, mwaka huu katika kikao cha pande hizo mbili kikiongozwa na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, George  Nyamaha.

Wafanyabiashara hao baada kuridhishwa na maelezo yake akisaidiwa na wataalamu kadhaa akiwemo na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Ester Chagulanya wamekubali kuanzia sasa watalipia  pango ya Sh200,000 kwa mwaka.

Makubaliano hayo yamewezesha vibanda hivyo kuwa mali ya halmashauri tangu vijengwe miaka 39 iliyopita.

Nyamaha katika maelezo ya awali aliyotoa wakati akifungua kikao alitaka suala hilo lifikie mwisho kwa sababu linaikosesha mapato halmashauri na kuwa ni miongoni mwa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Ndugu zangu mnatakiwa kulipa pango la vibanda hivyo ambapo halmashauri itapata mapato lakini pia tutaondokana na hoja ya CAG ya kutokusanya chanzo hicho cha mapato,” alisema.