Wafanyabiashara India waombwa kununua korosho

Muktasari:

  • Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Edwin Muhede amewataka wafanyabiashara na wawekezaji kutoka India waje kununua korosho na kujenga viwanda vya kubangua korosho.

Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Edwin Muhede amewataka wafanyabiashara nchini India kuja kununua korosho Tanzania na kujenga viwanda vya kubangua korosho.

Mwaka jana Serikali ilinunua korosho kutoka kwa wakulima baada ya wafanyabishara kugoma kununua korosho kwa bei elekezi ya Sh3,600 na badala yake walitaka kununua kwa bei Sh2, 600 jambo ambalo lilizua mzozo.

Dk Muhede, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda katika mkutano wa kibiashara baina ya wafanyabiashara kutoka India na nchi za Afrika Mashariki uliofanyika jijini hapa leo Alhamisi Machi 14, 2019 kuhusu India kuwekeza Tanzania, alitumia pia nafasi hiyo kuwahimiza wafanyabiashara hao kuja kununua korosho.

 

"Tunaomba  mje kununua korosho zipo za kutosha, Ili kupata utaratibu wa namna ya kuzinunua tunaomba mtembelee ofisi za wizara ili kupewa utaratibu mzuri,’’ alisema.

Dk Muhede pia alisema sera ya Serikali ni kujenga viwanda, aliwataka waje kuwekeza katika sekta ya viwanda kwani imeandaa mazingira rafiki ya uwekezaji na nchi ina amani ya kutosha huku akidai kwa sasa kipaumbele kikubwa ni kujenga viwanda vya kubangua korosho.