Wafanyabiashara Mwanza wajitokeza wiki ya mlipakodi

Wednesday May 15 2019

By Jesse Mikofu, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Wakati Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  ikiendelea kutoa elimu ya mlipa kodi, mwitikio wa wafanyabiashara si mkubwa.

Akizungumza katika eneo la Rwagasore jijini hapa leo Jumatano Mei 15, 2019 ofisa huduma na mlipa kodi wa TRA Mkoa wa Mwanza,  Lutufyo Mtafya amesema kwa siku wanahudumia watu kati ya 60 hadi 100.

“Siku ya kwanza tulihudumia watu takriban 60, siku ya Jumanne tulihudumia takriban watu 100 leo tunaendelea lakini mwitikio ni mzuri licha ya kuja mtu mmoja mmoja na kupata elimu kisha anaondoka ndio maana unaona hata hapa kwenye hema hakuna watu wengi,” amesema Mtafya.

Amesema watu wengi waliojitokeza katika huduma hiyo wanaonekana kuhamasika na ulipaji kodi ya majengo hasa wanataka kujua namna ya kulipia kwa njia ya simu.

Mmoja wa wananchi, Mussa Manyile amesema hatua hiyo imepunguza msongamano wanaoupata katika ofisi za mamlaka hiyo.

Akizungumzia utoaji wa risiti, mmoja wa wafanyabiashara, Said Tembo amesema wakati mwingine wanashindwa kutoa stakabadhi kutokana na matatizo ya mtandao na kuiomba TRA kufanyia marekebisho ya kiufundi ya mtandao wao.

Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa TRA, Rachel Mkundai, amesema mamlaka  hiyo inatumia fursa hiyo kusikiliza malalamiko, kupokea maoni, changamoto na mapendekezo kutoka kwa walipa kodi.

Kuanzia Mei 13, 2019 maofisa wa TRA wanaendesha kampeni ya elimu kwa umma kuwaelimisha wananchi kuhusu kodi ya majengo, Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat), kodi ya mapato, usajili wa walipa kodi wapya na namna yakulipa kodi kielektroniki.

Advertisement