Wafanyabiashara wa Kariakoo wafurahia elimu ya mlipakodi

Wednesday May 15 2019

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa soko la Kariakoo wamefurahia uwepo wa wiki ya mlipa kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa maelezo kuwa wamepata fursa ya kupata elimu kuhusu kodi ambayo awali walikuwa hawaijui.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Mei 15, 2019 eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam mmoja wa wafanyabiashara, Hamimu Abdullah amesema, “Ninafanya biashara ndogo hapa si rahisi kupata muda kwenda ofisi za TRA kupata elimu hii lakini ikitufuata kwa karibu hapa tunapata wasaa wa kufahamu mambo muhimu.”

Amesema sasa itakuwa rahisi kwake kufanya malipo ya kodi ya jengo na kwa kuwa hana muda wa kutosha atamuelekeza mke wake.

Mfanyabiashara mwingine, Joel Rubert amesema amefika eneo hilo ili kujiandikisha na kupata namba ya mlipa kodi lakini kwa kuwa haitolewi ameelekezwa mahali na namna ya kuipata.

"Nimekuja hapa ili kujiandikisha kama mlipa kodi mpya, maofisa hawa wamenielekeza niende ofisi za TRA karibu na nyumbani nitapatiwa huduma huko," amesema Rubert.

Maofisa wa TRA katika vituo hivyo vya huduma wanasema wao wanatoa elimu tu na kupokea maoni na iwapo mtu atahitaji huduma ya kiofisi anaelekezwa iliyo karibu naye na utaratibu wa kufuata.

Jana mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipa kodi wa TRA, Richard Kayombo alilieleza Mwananchi kuwa mwitikio wa watu ni mzuri mpaka sasa isipokuwa kwa mkoa wa Dar es Salaam kutokanana mvua zinazonyesha.

 “Hivi sasa niko Dodoma katika shughuli hiyo na jana tumezindua Arusha kwa kweli tumepata kuungwa mkono na viongozi wa wilaya na mikoa yote, mambo yanakwenda vizuri wafanyabiashara na walipa kodi wanafurahia huduma na wanajieleza kwa uhuru,” alisema.

Amesema baadhi ya maeneo wafanyabiashara wamependekeza elimu hiyo ingetolewa katika wilaya zote.

“Wengi wao wanauliza kuhusu kodi ya majengo, namna ya kulipa kodi mbalimbali, namna makadirio ya kodi yanavyofanyika, namna ya kulipa madeni mbalimbali ya kikodi na kutoa maoni yao na mapendekezo ya kuboresha (bila kutaja mapendekezo hayo),” alisema.

Advertisement