Wafanyakazi wamuokoa bosi

Meneja biashara wa kampuni ya nguzo ya New Forest, Dan Burton akiwa katika gari la polisi tayari kupelekwa kituoni baada ya kukaidi amri ya mkuu wa  Mkoa wa iringa, Ally Hapi ya kuruhusu magari kusafirisha nguzo akidai wanamtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenda kutoa taarifa hiyo. Picha na Pamela Chologola

Muktasari:

  • Katika majibu yake alimweleza mkuu wa mkoa kuwa hawatatoa magari ya kusafirisha nguzo hadi aende Waziri Mkuu

Iringa. Baaada ya kuitwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kueleza sababu za kuzuia nguzo za umeme kusafirishwa, mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi nusura amsweke mahabusu meneja biashara wa kampuni ya New Forest, Dan Burton baada ya kumjibu hawawezi kusafirisha nguzo hadi tamko la waziri mkuu.

Burton, jana alimweleza Hapi alipotembelea viwanda vinavyochakata nguzo za umeme na kujua sababu za kampuni hizo kutoruhusu magari kusafirisha nguzo, kuwa hawatazisafirisha hadi waziri mkuu aende kutoa tamko.

Baada ya maelezo hayo, Hapi aliamuru kamanda wa polisi mkoani hapa kuondoka na meneja huyo kutokana na majibu yake kwa maelezo kuwa amedharau sheria.

Hata hivyo, meneja huyo alinusurika baada ya kuombewa msamaha na wafanyakazi wake huku akiwa ameshakaa kwenye gari la polisi.

Hapi alisema waziri mkuu tayari ameelekeza kampuni zote kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na yeye (Hapi) amepewa jukumu la kusimamia.

Akijibu sababu za kutolipa, mhasibu wa kampuni hiyo Hosea alisema imetokana na mkurugenzi wa mtendaji wa Wilaya ya Kilolo kuwa kwenye mawasiliano na mkurugenzi kampuni.

Hata hivyo, Hapi aliamua kumpigia simu mkurugenzi wa Kilolo kutaka kujua sababu za kutolipwa ambaye alieleza kuwa wameahidi kulipa Ijumaa hii.

Wakati mkuu wa mkoa akiendelea kukagua kiwanda alibaini magari 26 wakiwa yamesheheni nguzo yamezuiwa kutoka kwa maelezo kuwa hawajafikia mwafaka.

Pia, wafanyakazi wamepewa likizo kwa muda usiojulikana kutokana na kampuni kusimama mapaka itakapofikia mwafaka wa kulipa kodi.