Wafungwa 3, 530 wapata msamaha wa Rais

Friday April 26 2019

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa wakiwamo wenye maradhi ikiwamo ukimwi, kifua kikuu na saratani.

Kwenye msamaha huo waliosamehewa ni wafungwa 3, 530, ambapo 722 wataachiwa huru leo na 2, 808 watabaki gerezani kumalizia sehemu ya kifungo kilichobaki baada ya kupewa msamaha huo.

Magufuli ametoa msamaha huo leo Aprili 26 ikiwa ni kuadhimisha miaka 55 ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya ibara ya 45 (1)(d) ya katiba ya Tanzania.

Mbali na wafungwa hao, Rais Magufuli pia ametoa msamaha kwa kuelekeza wafungwa wote wapunguziwe robo ya adhabu zao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu linalotolewa chini ya kifungu 49(1) cha Sheria ya magereza Sura ya 58.

“Wafungwa hao sharti wawe wametimiza robo ya adhabu zao gerezani isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika ibara ya 2 (1-xxi)” imesema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu.

Mbali ya hayo taarifa hiyo imesema msamaha huo pia utawahusu wafungwa walioingia gerezani kabla ya Machi 15 mwaka huu.

“Msamaha utawahusu wafungwa wagonjwa wa ukimwi, saratani, kifua kikuu ambao wapo kwenye hatua za mwisho za ugonjwa na wathibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa na wilaya,” imesema taarifa hiyo.

Rais pia amewasamehe wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 na zaidi lakini umri huo uthibitishwe na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa na wilaya.

Pia waliosamehewa ni wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

Rais Magufuli pia amewasamehe wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili  lakini uthibitishwe na waganga   chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa na wilaya.

Taarifa hiyo imeeleza msamaha huo hautawahusu wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa au kwa makosa ya kujaribu kuua, kujaribu kujiua au kuua watoto.

Rais pia hajawasamehe wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani na wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

Pia wafungwa ambao wanatumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya kama cocaine, heroin na bangi hawahusiki na msiba huo.

Msamaha wa Rais pia hautawahusu wafungwa wanaotumia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji, upokeaji au utoaji rushwa.

“Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo pia hawatahusika,” imesema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:

“Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au mlipuko isivyo kihalali nao pia hawamo”.

Wafungwa wengine ambao msamaha huo hauwahusu ni wanatumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka, kulawiti, ukatili dhidi ya watoto au kujaribu kutenda makosa hayo.

Pia waliohukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na za sekondari ambao walitenda kosa wakiwa na miaka 18 na kuendelea hawatahusika.

Rais hajawasamehe pia wafungwa wanaotumikia kifungo kwa amkosa ya wizi wa magari, pikipiki na uharibifu wa miundombinu.

Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao, utakatishaji fedha na uhujumu uchumi na waliowahi kupunguziwa kifungo na Rais ambao bado wanaendelea na kifungo kilichobakia.

Wafungwa wengine ambao hawatahusika na msamaha huo ni wale waliokatisha haki ya watoto kupata masomo, waliohusika kwenye utekaji watoto, ukatili dhidi yao, kupoka na kufanya biashara ya binadamu.

Taarifa hiyo imeleza pia waliohukumiwa kwa makosa ya kukutwa na viungo vya binadamu, nyara za Serikali na ujangili hautawahusu.

Imesema wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi, ubadhilifu wa fedha za Serikali na makosa ya kutoroka chini ya ulinzi halali au kusaidia kutendeka makosa hayo hawahusiki.

“Wafungwa waliowahi kufungwa na kurudia kufungwa tena  na wenye makosa ya kinidhamu gerezani pia hawamo katika msamaha huo,” imesema taarifa hiyo.

Advertisement