Wafurahia kuanzishwa soko la madini

Muktasari:

Wachimbaji wadogo wa madini Morogoro wamefurahishwa na uanzishwaji wa soko la madini katika mkoa huo huku wakihimizana kuacha kuficha.

Morogoro. Wachimbaji wadogo wa madini mkoani Morogoro wamesema uanzishwaji wa masoko ya madini ni ukombozi kwao na utawaongezea tija ya uzalishaji na kuongeza kipato huku wakiwasihi wenzao kuacha kuficha madini nyumbani.

Wachimbaji hao kutoka maeneo tofauti ya wilaya za Morogoro, wametoa kauli hiyo leo Jumapili Mei 19, 2019 wakati wa uzinduzi rasmi wa soko la madini lililozinduliwa na Mkuu wa Mkoa huo, Dk Steven Kebwe.

Naibu katibu mkuu wa chama cha wachimbaji wadogo wa madini mkoani Morogoro (Morema), Elizabeth Chuwa amesema Rais John  Magufuli aliwaza mbali katika kuhakikisha masoko hayo yanaanzishwa.

Amesema kitu cha msingi na kuzingatiwa kwa sasa ni kuhakikisha hayapotei kama zamani.

Amesema kuwepo kwa masoko hayo kutakomesha utoroshwaji wa madini nje ya nchi ambao ulikuwa unawanufaisha wachache na si Taifa.

“Sisi wachimbaji wadogo tunampongeza Rais kwa kufanya uamuzi huu wa kuwapo kwa masoko katika kila mkoa, itatusaidia sisi wadogo ambao tulikuwa tunadhulumiwa,” amesema Chuwa.

 

Akizindua soko hilo, Dk Kebwe amesema litasaidia kuondoa kudhulumiwa kwa wachimbaji wadogo tofauti na awali.

Dk Kebwe amesema kwa sasa wachimbaji watakuwa na uhakika wa soko huku akieleza kuwa mkoa unaendelea kuimarisha mifumo yake ya kiuchumi pamoja na suala la masoko ya madini na bidhaa mbalimbali za mazao.

Mkuu huyo wa mkoa aliwataka wachimbaji kutumia vyema masoko yanayofunguliwa na kuwatahadharisha kutokaa na madini zaidi ya siku tano pindi wanapoyachimba na kutakiwa kuyapeleka sokoni ili yahifadhiwe huko.

“Kama mchimbaji ataonekana kukaa na madini nyumbani zaidi ya siku tano, ajue sheria itachukua mkondo wake kama inavyoelekeza na kwa kufanya hivyo, utaonekana umekiuka taratibu zilizopo za madini,” amesema Kebwe.