Wagombea tisa wachukua fomu kumrithi Nassari

Muktasari:

  • Vyama tisa vimechukuwa fomu za kugombea ubunge jimbo la Arumeru Mashariki kurithi kiti cha ubunge kilichowachwa wazi na mbunge wa jimbo hilo, Joshua Nassari ambaye alivuliwa ubunge  baada ya kutohudhuria mikutano mitatu mfululizo ya bunge.

Arumeru. Vyama tisa vimejitokeza kuchukua fomu za kugombea ubunge katika jimbo la Arumeru Mashariki, uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika  Mei 19, huku utata ukiibuka kwa wagombea wa vyama vya CUF na DP ambavyo wamejitokeza wagombea wawili wawili wakiwa na barua za utambulisho kuchukua fomu.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya Bunge la Tanzania kutangaza mbunge wa jimbo hilo Joshua Nassari (Chadema) amepoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na kutokuhudhuria vikao vya mikutano mitatu bila taarifa kinyume cha sheria.

Msimamizi wa uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo la Arumeru Mashariki,  Immanuel  Mkongo  akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Aprili 18,2019, amesema wagombea  ambao wamechukua fomu  ni kutoka NCCR – Mageuzi,   SAU, na Tadea.

Wagombea wengine ambao wamechukua fomu ni wa Chama cha  Demokrasia Makini, Alliance for Africa Farmers Party  ( AAFP), United People Democract Party  (UPDP), Nation Reconstruction  Alliance (NRA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Emmanuel amesema shughuli ya kuchukua fomu na kurejesha linatarajiwa kukamilika kesho Ijumaa Aprili 19, ambapo tume ya uchaguzi itatangaza majina ya wagombea waliokidhi masharti.

Amesema kuna changamoto ambazo zimejitokeza katika shughuli hiyo ya uchukuaji wa fomu kwani  kuna vyama viwili, CUF na DP ambavyo vimepeleka wagombea wawili badala ya mmoja kila chama.

“Nimewarudisha waje na mgombea mmoja baada ya kukubaliana ndani ya vyama vyao kabla ya siku ya mwisho.”

“Baada kupitisha wagombea,  kampeni zitaanza Aprili  20 mpaka Mei 18  kwa wale watakao fanikiwa  kuteuliwa kwa ajili ya uchaguzi na uchaguzi utafanyika  Mei 19,” amesema.

Mgombea wa Demokrasi Makini, Simon Ngilisho amesema amejipanga kufanya kampeni za kisasa na hivyo kuibuka na ushindi katika uchaguzi huo.

“Nimepitishwa na chama kugombea ubunge na nina imani nitakamilisha taratibu zote ili kupitishwa na tume na hivyo kushiriki uchaguzi huu vizuri,” amesema.

Mjumbe wa mkutano mkuu wa CUF, Abdalah Shabani amekiri kuibuka mgogoro juu ya wagombea lakini akasema wameshangazwa na mgombea ambaye hajapitishwa na chama hicho kwenda kuchukua fomu.