Wahoji hatua dhidi ya wauaji wa mwanamke Rombo

Muktasari:

Paroko wa Parokia ya Usseri, Padri Emmanuel Liyimo amekemea tukio la mwanamke kuuawa wilayani Rombo na kuiomba Serikali ichukue hatua huku mbunge wa Rombo Joseph Selasini akisema kwamba tukio hilo ni la kikatili na la aibu.

Rombo. Mbunge wa Rombo na Paroko wamezungumzia sakata la mwanamke kuuawa wilayani Rombo kwa madai ya mwanaye kuiba chakula kwa jirani na kukila.

Mwanamke huyo, Adelaide Onesmo wa Kijiji cha Lessoroma, aliuawa kwa kupigwa hadi kufa Februari 11 na wanawake wenzake wanaodaiwa kuwa sita wakimtuhumu mwanaye anayesoma darasa la sita kuiba chakula maarufu kwa Wachaga, Ngararimo.

Akizungumzia tukio hilo, Joseph Selasini alisema ni la kikatili na ni la aibu na kwamba yameendelea kushamiri wilayani humo kutokana na Jeshi la Polisi kushindwa kulinda usalama wa raia.

Selasini ambaye ni mbunge kwa tiketi ya Chadema alisema inasikitisha kuona hadi sasa wanawake hao hawajakamatwa ilhali mtoto anayetuhumiwa ameshawataja na kuwaonyesha wahusika wanaodaiwa kushiriki mauaji hayo.

“Haya matukio ya ukatili yamekithiri sana Rombo na sijui kwa nini polisi wanashindwa kufanya kazi yao na kuchukua hatua.

Alisema kama wanawake hao wanaodaiwa kumpiga mwenzao wameshatajwa na mtoto aliyedaiwa kuiba chakula hicho aliwaonyesha na jana ilikuwa siku ya tano huku wakiwa hawajakamatwa, alisema kinaashiria kitu ndani ya Jeshi la Polisi.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu madai hayo, Kamanda Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema hawajafumbia macho mauaji hayo na kwamba wanaendelea na uchunguzi kuwabaini wahusika.

Licha ya majibu ya kamanda huyo wa polisi, Selasini aliendelea kulitupia lawama jeshi hilo akilitaka lijitathmini katika utendaji wake wa kazi akidai kwamba katika Wilaya ya Rombo, mtu akiwa na nguvu ya fedha ndipo polisi wanafanya kazi.

Akihubiri jana katika misa takatifu ya Jumapili, Paroko wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Usseri, Emmanuel Lyimo alisema kuna haja kwa Serikali kuanza kutumia nguvu za ziada kupambana na matukio ya mauaji na ukatili yanayotokea katika wilaya hiyo ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumzia tukio hilo la kuuawa kwa mwanamke huyo, Padri Lyimo alisema ni la kinyama na halipaswi kufumbiwa macho na jamii.

Alisema wimbi la watu kujichukulia sheria mkononi na kuua wengine linazidi kushika kasi huku vitendo vya ubakaji na ulawiti navyo vikiendelea kushamiri.

“Haya mauaji yanayofanywa Katika Tarafa hii ya usseri pamoja na sehemu nyingine, hakika hizi damu za watu zinazomwagika zitawalilia watu wa Usseri,” alisema Paroko huyo.

Mkazi wa Usseri, Amani Karimu alisema matukio yanayoendelea wilayani humo yanazidi kuwajengea hofu ya usalama wao.

“Watu tumekua na hofu ya kusema, uongozi upo hawasemi, Polisi wanapeleleza mambo juujuu tu na baadhi yao wanaonekana kuegemea upande wenye masilahi yao. Hebu angalia hii familia ingekua na watu wenye uwezo, hawa watuhumiwa wangekuwa wameshakamatwa,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Agness Hokororo alipoulizwa hatua zilizochukuliwa na Serikali kukabiliana na matukio hayo alisema, “unataka nikuambie nini wakati mmeshaandika. Sina cha kusema kwanza naenda kwenye ziara ya naibu waziri.”

Mwili wa mwanamke huyo bado umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Karume wilayani Rombo.