Waitara awataka maofisa elimu kuingia darasani kufundisha

Muktasari:

  • Naibu Waziri Waitara awataka maofisa elimu Tanzania kuingia darasani kufundisha katika maeneo yao

Babati. Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara amewataka maofisa elimu nchini kuingia darasani na kufundisha wanafunzi kwenye shule zilizo maeneo yao.

Waitara ameyasema hayo kwenye Uwanja wa Kwaraa mjini Babati mkoani Manyara leo Jumamosi Aprili 6, 2019 wakati akizindua mashindano ya Shule za Sekondari (Umiseta) ngazi ya Taifa.

Naibu waziri huyo amesema maofisa elimu hao wanapaswa kufundisha shule zilizo karibu na maeneo yao ya kazi kwani ni taaluma zao.

Waitara amesema maofisa elimu hao wanapaswa kujipangia vipindi kwenye shule za msingi na sekondari ambazo zina upungufu wa walimu.

"Hata mimi jimboni kwangu Ukonga huwa nafundisha baadhi ya masomo hasa ya sayansi na hisabati hivyo na ninyi igeni hilo," amesema Waitara.

Mmoja kati ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Babati Day, Josephina Boay amesema agizo hilo la Naibu Waziri Waitara limekuja kwa wakati muafaka kwani hivi sasa shule nyingi zina changamoto ya upungufu wa walimu.

Mwanafunzi mwingine John Martin amesema hatua hiyo itachangia kupanda kwa taaluma kwani wanafunzi watafurahi kufundishwa na maofisa elimu.

Katika uzinduzi huo shule 18 za Serikali na za binafsi zimeshiriki mashindano hayo yanayotarajiwa kukamilika mkoani Mtwara mwezi Juni mwaka huu.