Wajane wamiminika kwa Makonda

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Paul Makonda leo Alhamisi ameandaa kongamano ambalo linawakutanisha wajane wa mkoa huo kujadili masuala mbalimbali ikiwamo ya kisheria

Dar es Salaam. Wanawake wajane wamefurika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam kumsikiliza mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda.

Wanawake hao wamejaa katika ukumbi mkubwa wa mikutano na wengine kwa idadi kama hiyo wakiwa wamejazana nje baada ya kuzuiwa kuingia ndani.

Makonda amewaita leo Alhamisi Aprili 4, 2019 wanawake hao katika kongamano maalumu ambalo pamoja na kuongea nao litatumika kutoa elimu mbalimbali ikiwamo kujitambua na ujasiriamali.

Wanawake walio nje wanalalamika kukosa nafasi na kuomba kongamano hilo lifanyike katika viwanja vya wazi kutokana na idadi kubwa iliyopo.

"Nimekuja tangu saa mbili lakini nimeishia nje, binafsi nimekuja kwa sababu baada ya kufiwa nilipokonywa kila kitu na nimepoteza mwelekeo wa maisha," amesema Fatma Almasi mkazi wa Congo la mboto.

Kinachoendelea sasa ukumbini ni burudani kutoka kwa mwimbaji wa taarabu, Hadija Kopa.