Wajumbe 32 kutoka SADC wakutana Tanzania kaujadili sekta ya afya

Wednesday August 14 2019

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wajumbe 32 kutoka  nchi 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), wamekutana Tanzania kwa mafunzo ya siku 14 kwa lengo la kujifunza mifumo bora ya uzalishaji bidhaa za dawa na vifaa tiba.

Uwepo wa mafunzo hayo utasaidia nchi wanachama kutumia wataalamu wake waliopewa mafunzo kwenda katika viwanda vya dawa kufanya ukaguzi wa pamoja na kusajili dawa kwa pamoja katika nchi zote 16 ikiwa ni katika mkakati wa manunuzi ya pamoja ya dawa.

Kwa mujibu taarifa iliyotolewa leo Jumatano Agosti 14, 2019 mafunzo hayo yana lengo la kusaidia udhibiti wa dawa zisizo na viwango kuingia katika nchi hizo 16.

Akizindua mafunzo hayo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Tanzania, Dk Zainabu Chaula amesema Tanzania imepiga hatua kubwa na kupata cheti cha mifumo bora ya usimamiaji wa dawa na bidhaa zitokanazo na dawa katika nchi za Afrika na hilo limesababisha nchi za SADCc kuiteua Tanzania kusimamia manunuzi na kutumika kufundishia wataalamu.

Amesema hiyo itasaidia nchi zingine 15 kudhibiti dawa zisizo na viwango, feki kuingia nchini kwao kuanzia sehemu za mipakani.

“Nchi yetu imepiga hatua kubwa tumetunukiwa cheti cha mifumo bora kwa usimamiaji wa ubora wa dawa na vifaa au bidhaa zitokanazo na dawa kwa Afrika.”

Advertisement

“Nchi yetu mwaka huu inasimamia mkutano mkuu wa SADC wa 39 na kwakuwa elimu kubwa ipo Tanzania, tumeona tuendeshe mafunzo haya ili  nchi wanachama wawe na uelewa wa pamoja,” amesema Dk Chaula.

Advertisement