Wakandarasi wasio na sifa kufutwa

Msajili wa Bodi ya usajili wa makandarasi (CRB) Rhoben Nkori akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari juu ya uhakiki wa utendaji kazi, sifa za  wakandarasi nchi nzima.

Muktasari:

Bodi ya usajili wa wakandarasi itachukua hatua hiyo ikiwa ni mara ya kwanza nchini baada ya kuona Serikali inaingiza fedha nyingi kwenye miradi wanayopewa kazi wazawa lakini kunakuwa na matatizo.

Dar es Salaam. Wakandarasi wasiokuwa na sifa watafutiwa usajili wao na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi Tanzania (CRB).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mei 24, 2019, msajili wa bodi ya usajili ya  wakandarasi, Rhoben Nkori amesema kuwa wameona ni wakati muafaka wa kuchukua hatua hiyo ili kubaini wakandarasi waliopoteza sifa, kutokana na kukithiri kwa malalamiko ya kutofanya kazi zao kwa viwango stahiki.

Amesema kuwa kumekuwa na malalamiko ya  baadhi ya wakandarasi kushindwa kutimiza wajibu wao kama vile kuchelewesha kazi , kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi, kukimbia kazi pamoja na kutoa gharama zisizomithilika.

 “Ukisikiliza taarifa ya habari kwenye runinga, ukisoma magazeti, kila kukicha wakandarasi wanaharibu kazi, wananyang’anywa, wanakimbia miradi, kupitia uhakiki huu tutawaengua wale wanaofanya ujanja ujanja”amesema Nkori.

Amesema kuwa baada ya uhakiki  huo yatafanyika mambo mawili ambayo ni kushushwa madaraja yao ya usajili au kufutwa kabisa.

“Hatua hiyo ya uhakiki maalumu awamu ya kwanza itaanza Mei 27, 2019 hadi Julai 20, 2019 ambapo wataanza wakandarasi wakubwa wa daraja la kwanza hadi la tatu, ikijumuisha na makandarasi maalumu daraja la kwanza.

“Awamu ya pili itaanza Agosti hadi Novemba 15, 2019 ambayo itahusisha wakandarasi wa daraja la nne hadi la saba ikijumuisha wakandarasi maalumu wa daraja la kwanza na la pili”amesema Nkori.

Amesema mambo wanayoangalia ni uwezo wao ikiwamo wataalamu waliokuwa nao wakati wanasajiliwa, miradi waliyofanya kwa ufanisi na uwezo wa vifaa walivyonavyo.

Amefafanua kuwa wanachukua hatua hiyo baada ya kuona Serikali inaingiza fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali ambayo wanapewa kazi wakandarasi wazawa ambao kwa sababu moja ama nyingine hawafanyi kazi zao kwa ufanisi.

“Wanaitia hasara serikali, wanatumia vibaya kodi za wananchi, hivyo tunawafanyia uhakiki na watakaobainika hawana sifa kabisa tunawafutia usajili na watakaopungukiwa vigezo tunawashusha madaraja,”amesema Nkori.

Amefafanua kuwa kila mara huwa wanapitia utendaji wa wakandarasi waliosajiliwa na Bodi, lakini kwa kuwapa fomu wajaze na kueleza shughuli zao wao wenyewe,  lakini katika uhakiki huo maalumu wanakwenda kuonana nao ana kwa ana kujionea vifaa na wataalamu walio nao.

“Uhakiki kama huu ni mara ya kwanza, na watakaobainika kuwa walipata miradi kwa njia ya rushwa (ikithibitishwa na vyombo husika), walifoji nyaraka za miradi yao, na wasio na uwezo ikiwamo kukosa wataalamu, kutotoa ushirikiano wakati wa uhakiki na kuwa na vifaa duni, watafutiwa usajili wao, ”amesema.

Nkori alitaja miradi ambayo imekuwa ikilalamikiwa sana kuwa chini ya kiwango licha ya wakandarasi wazawa kupewa kazi hizo ni ujenzi wa barabara, hospitali na vituo vya afya, miradi ya maji ambayo ndiyo mingi imekuwa sugu.

 “Kutokana na unyeti wa uhakiki huo Bodi imeandaa utaratibu utakaowezesha kuwafikia wote nchi nzima, ombi langu ni makandarasi kutoa ushirikiano kwa maofisa wa bodi watakapokuwa wanatekeleza hatua hiyo”alitoa rai Nkori.