Wake za Rais, naibu Rais waongezewa dau nono

Muktasari:

Ofisi ya mke wa Rais Uhuru Kenyatta, Margaret Kenyatta na ya Naibu Rais William Ruto zimetengewa Sh723.6 milioni (Sh15.9 bilioni za Tanzania)  kwenye bajeti ya mwaka 2019

Nairobi, Kenya. Ofisi ya mke wa Rais Uhuru Kenyatta, Margaret Kenyatta na ya Naibu Rais William Ruto zimetengewa Sh723.6 milioni (Sh15.9 bilioni za Tanzania)  kwenye bajeti ya mwaka 2019.

Kiasi hicho ni mara tatu zaidi ya fedha ambazo afisi za Margaret Kenyatta na Rachael Ruto walitengewa mwaka 2013.

Fedha hizo zitaanza kutumiwa kwenye mwaka wa fedha 2019/2020 utakaoanza Julai.

Kulingana na taarifa ya makadirio ya fedha za serikali kutoka kwa Hazina ya Kitaifa, kiasi kikubwa cha fedha hizo kitatumika kulipia mishahara ya wafanyakazi, kugharimia usafiri na burudani.

Wawili hao walipokea Sh187.3 milioni mwaka 2013. Bajeti ya afisi ya mke wa rais imeongezeka kutoka Sh114.4 milioni hadi Sh426.1 milioni, ile ya mke wa Ruto imeongezeka kutoka Sh72.9 milioni hadi Sh297 milioni.

Ongezeko hilo linajiri huku Rais Kenyatta akizidi kutoa miito kwa idara mbalimbali za serikali kupunguza matumizi ya fedha katika masuala yasiyo muhimu kama vyakula na safari.

Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali ilitoa maagizo kuwazuia maafisa wake wakuu dhidi ya kusafiri nje ya nchi bila ruhusa maalumu kutoka kwa Rais. Serikali pia imekuwa ikifuatilia sana safari za maeneo mbalimbali humu nchini.

Gazeti la Taifa Leo linasema haya yanajiri huku Wakenya wakiendelea kulalamikia ugumu wa maisha.

Wadadisi wa masuala ya kiuchumi pia wamekuwa wakilalamikia mtindo wa serikali kuchukua mikopo kutoka nchi za nje, hasa China, wakionya kuwa ni mojawapo ya sababu ambazo zimemwongezea mwananchi mzigo.