Wakili Takukuru akwamisha kesi vigogo TRL

Muktasari:

  • Kukosekana mahakamani kwa wakili wa Takukuru, Moghela Ndimbo kumesababisha kesi inayowakabili vigogo 18 wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kupigwa kalenda

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea na ushahidi wa kesi inayowakabili vigogo 18 wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) baada ya wakili  wa Takukuru, Moghela Ndimbo anayeendesha shauri hilo kupata udhuru.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni pamoja na aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Kipallo Kisamfu wanaokabiliwa na mashtaka 15 ya matumizi mabaya ya madaraka.

Wakili wa taasisi hiyo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ,Imani Mitume ameieleza mahakama leo Jumatano Julai 3, 2019 mbele ya hakimu mkazi mfawidhi, Kelvin Mhina  kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya kusikilizwa, kwamba  wakili anayesimamia kesi hiyo amepata udhuru na kuomba tarehe nyingine.

Baada ya maelezo hayo hakimu Mhina amesema shauri hilo litasikilizwa kwa siku tatu mfululizo na kuahirisha kesi

hadi Agosti 14, 15 na 16, 2019.

Katika kesi hiyo, washitakiwa wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuingia mikataba ya zabuni ya ununuzi wa vichwa vya treni na kuipa zabuni hiyo kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries Limited.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo  kwa nyakati tofauti kati ya Oktoba 23, 2012 na Aprili 26, 2015.

Mbali na Kisamfu wengine ni mkuu wa kitengo cha makenika na mhasibu mkuu, Jasper Kisiraga; kaimu meneja wa usafiri, Mathias Massae; kaimu mhandisi wa ufundi na meneja ujenzi, Muungano Kaupunda na mkuu wa ufundi na meneja ujenzi, Ngoso Ngosomwiles.

Wengine ni mhandisi mkuu wa ufundi, Paschal Mafikiri;  mhandisi mipango,  Kedmo Mapunda;  kaimu mhandisi wa mawasiliano, Felix Kashaingili; mkuu wa usafiri wa reli, Lowland Simtengu; mkuu wa ubunifu na utengenezaji wa nyaraka, Joseph Syaizyagi na kaimu mkuu wa usafirishaji, Charles Ndenge.