Wakili ahofia Msajili kuwa na madaraka makubwa kuliko Rais

Saturday January 12 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakili maarufu nchini, Harold Sungusia amesema Muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa wa mwaka 2018 ukipita kuwa sheria, msajili atakuwa na madaraka makubwa kuliko Rais.

Amesema madaraka ya msajili wa vyama vya siasa utamfanya Msajili kuwa na madaraka makubwa kuliko Rais wa Jamhuri ya Muungano, huku pia akihoji kinga atakayopewa ya kutokushitakiwa.

Akizungumza leo Jumamosi Januari 12, 2019 katika mjadala wa wazi ulioandaliwa na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), jijini Dar es Salaam, Sungusia amesema muswada huo unapora madaraka ya wananchi kikatiba.

"Msajili anaweza kuamua usajiliwe au usisajiliwe, ufutwe au usifutwe, uwe mwanachama au sio, unafaa kuwa mgombea au hufai, aina gani ya elimu ya uraia inayotakiwa na nani atoe, upewe ruzuku au usipewe," amesema Sungusia.

"Je, akimfuta uanachama Rais? Yaani msajili ana mamlaka kuliko Rais. Ni jambo kubwa la Kikatiba," ameongeza.

Ameendelea kutaja Kifungu cha 6 kinachompa kinga Msajili, Sungusia amesema kwa sheria ya sasa angeweza kushitakiwa kwa makosa ya uzembe lakini kwa muswada mpya hashitakiwi kabisa. "Kinga lazima iendane na Katiba na haki za binadamu," amesema Sungusia.

Akizungumzia utungwaji wa kanuni, Sungusia amehoji uhalali wa waziri huyo. "Waziri anatoka wapi, chama gani? Mnakumbuka kikokotoo, Waziri alitakiwa kutunga kanuni na akatunga kweli. Ukimwachia mwanafunzi atunge kanuni atafanyaje?" Amehoji

Kuhusu vyama vya siasa kutofanya harakati, Sungusia amesema hata chama cha TANU kilifanya harakati hadi uhuru ukapatikana.

"Sasa vyama vitakuwa kwaya za siasa. Kazi ya chama cha siasa ni kuchukua madaraka, huchukui madaraka kwa kuimba pambio. Hata TANU waliwashinikiza Wazungu wakatoa madaraka," amesema.

Baadhi ya wanajopo waliojadili sheria hiyo akiwemo Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza amesema muswada huo hauakisi matakwa ya vyama vya siasa bali ya msajili.

"Muswada una ujasiri mkubwa wa kuingilia haki za wengine. Kuna  hatari ya kujenga mazoea ya kuwa na ujasiri wa vyombo vingine kuingilia haki za wengine.

"Maana msajili amepewa haki, kama utapita kuna siku vyombo vingine vitaingilia haki ya kuabudu," amesema.

Advertisement