Wakili ajitoa kusimamia kesi baada ya kukosa ushirikiano

Wednesday August 14 2019

By Suzana Otaigo na Faraji Issah, Mwananchi.

Dar es salaam, Wakili wa utetezi, Castor Rweikiza amejitoa kusimamia shtaka linalomkabili mteja wake ambaye ni Charles Magita baada ya kukosa ushirikiano kutoka kwa ndugu wa mshtakiwa.

Wakili Rweikiza amejiondoa katika shtaka hilo leo jumatano Agosti 14,2019 mbele ya Hakimu Mkazi Caroline Kiliwa, katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni.

Alisema kuwa  ndugu wa mshtakiwa hawana ushirikiano kwakuwa hawafuatilii mwenendo wa kesi ya ndugu yao pia hawana mawasiliano mazuri kama walivyokubaliana hapo awali.

Akiongoza shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Caroline Kiliwa, Wakili wa Serikali, Neema Moshi amedai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na shtaka la ukabaji na kuiba simu aina ya Tecno phantom 6 yenye thamani ya 600,000 na pesa taslim 40,000 ambavyo ni Mali ya Sulemani Mshobozi Disemba mosi,2018 eneo la Goba Kulangwa jijini Dar es salaam.

Wakili wa utetezi amejiondoa kusimamia shtaka hilo hadi ndugu watakapoonesha ushirikiano kama walivyokubaliana hapo awali ."Ndugu hawana ushirikiano, hawapokei simu, shauri linaniingiza kwenye gharama sitaendelea na shauri hadi ndugu watakapo onesha ushirikiano".

Kwa upande wa mshtakiwa alipoulizwa  na wakili wake wa utetezi kuwa kwanini ndugu zake hawaoneshi ushirikiano akasema kuwa hata yeye haelewi na anashangaa kwanini hapewi ushirikiano na ndugu zake.

Advertisement

Hakimu Kiliwa alihairisha kesi hiyo hadi Agosti 28, 2019 kwaajili ya kusikilizwa tena na mshtakiwa amerudishwa rumande.

Advertisement