VIDEO: Bashe: Walichokifanya Kinana, Makamba ni kumkosesha Magufuli uhalali kuwania urais 2020

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe 

Muktasari:

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe amesema kitendo cha makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana kumuandikia barua katibu wa baraza la ushauri la viongozi wakuu wastaafu wa chama hicho wakilalamika kudhalilishwa, ni mkakati unaolenga kutaka kumkosesha uhalali Rais John Magufuli kuwania urais 2020


Dar es Salaam. Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe amesema kitendo cha makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana kumuandikia barua katibu wa baraza la ushauri la viongozi wakuu wastaafu wa chama hicho wakilalamika kudhalilishwa, ni mkakati unaolenga kutaka kumkosesha uhalali Rais John Magufuli kuwania urais 2020.

Bashe ametoa kauli hiyo leo Jumatano Julai 17, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Makamba alikuwa katibu mkuu wa sita na Kinana (wa nane) wametoa taarifa ya maandishi kwa umma Julai 14, 2019 ambayo wameisaini wakimlalamikia mtu anayejitambulisha kama mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.“Mara kadhaa ametutuhumu sisi wawili, makatibu wakuu wastaafu wa CCM kwa mambo ya uzushi na uongo,” inasema taarifa yao hiyo.

Wastaafu hao wanasema wametafakari kwa kina kabla ya kutoa taarifa kuhusu taarifa wanazodai za uzushi kwa nyakati mbili tofauti.

Walisema kwa sasa Watanzania wanajua kuwa yanayosemwa na mtu huyo si ya kwake.

Wanasema mara kwa mara Watanzania wamekuwa wakijiuliza kwamba mtu huyo, ambaye amemtaja lakini jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kitaaluma, anatumwa na nani?

Katika maelezo yake ya leo, Bashe amesema tamko la makatibu wakuu hao wastaafu walilomuandikia katibu wa baraza la ushauri la viongozi wakuu wastaafu, Pius Msekwa, limekwenda kinyume cha Katiba ya CCM.

“Hatuwezi kuruhusu Magufuli ni mwenyekiti wetu, ni mgombea wetu wa urais 2020, come sun come rain (lije jua ije mvua), hatuwezi kuruhusu hatua ambayo inadhoofisha uhai wa chama,” amesema Bashe.

Ametaja kifungu 122 (1) cha Kaiba ya CCM akisema kimekiukwa na tamko hilo kwa kuwa baraza hilo halina mamlaka ya kusikiliza malalamiko hayo.

“Ukiwa na malalamiko lazima ujue wa kumwandikia. Mimi nikilalamikia gazeti namwandikia editor (mhariri) ndio ana mamlaka ya kisheria, siwezi kumwambia circulation manager (meneja usambazaji),” amesema Bashe.

Amebainisha kuwa kosa jingine lililofanywa na makatibu hao kwenye waraka wao ni kuuweka hadharani.