Walimu wa hisabati wapewa neno

Muktasari:

  • Kwa mara ya pili Tanzania inaadhimisha siku ya hisabati baada ya kuacha kutumia jina la siku ya Pai ili kuhamasisha umuhimu wa somo hilo katika maendeleo ya taifa.

Dar es Salaam.  Wakati kilio cha wanafunzi wengi kufeli somo la hisabati kikiendelea, walimu wanaofundisha somo hilo wametakiwa kutokuwa chanzo cha kuwatengenezea hofu wanafunzi kuliogopa.

Badala yake wametakiwa kufundisha hesabu kwa upole na upendo huku wakiwaeleza wazi wanafunzi kuwa hesabu si ngumu.

Kwa miaka zaidi ya 10 mfululizo ufaulu wa hesabu kwa shule za sekondari upo chini ya asilimia 20 na kulifanya somo hilo kuwa la mwisho.

Katika maadhimisho ya siku ya hisabati duniani yaliyofanyika leo Alhamisi Machi 14, 2019 jijini Dar es Salaam, wadau wa somo hilo wakiwamo walimu na wanafunzi wamesimama na kushangilia saa 7:59:26 mchana kama ishara ya kuiambia dunia umuhimu wa hisabati.

Akizungumza, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu, Ofisi ya Rais, Julius Nestory amesema kitendo cha kuwajengea wanafunzi fikra mbaya kuhusu hisabati ni kati ya changamoto zinazokwamisha ufaulu wa somo hilo.

Alisema wanafunzi hujikuta wakikwepa hesabu wanapoogopeshwa na walimu wao kuwa hesabu ni ngumu wakati si kweli.

"Walimu wa hesabu msiwaogopeshe watoto kuwa hesabu ni ngumu, wafundisheni watoto kwa upendo na si somo gumu," amesema Nestory na kuongeza;

"Hesabu si ugonjwa wa taifa kama wengine wanavyofikiria, hesabu ni dawa ya taifa."

Aliwataka walimu kuelekeza nguvu zao katika kufundisha somo hilo kwa vitendo badala ya nadharia.

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania  (CHAT/CHAHITA)  Dk Sima Said amesema pamoja na jitihada nyingi zinazofanywa kuinua somo hilo bado hali ni mbaya.

"Mwaka 1970 ufaulu wa hesabu sekondari ulikuwa zaidi ya asilimia 50, tunatamani sana turudi huko walau basi tufikie asilimia 30 kuliko hii hali ya sasa," amesema.

Amesema hakuna uchumi wa viwanda unaoweza kufikiwa kama somo la hisabati litawekwa pembeni.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Aga Khan, Veronica Sarungi amesema kiuhalisia somo la hisabati halina ugumu wowote na kuna kila sababu ya kuhakikisha wanafunzi wanajifunza somo hilo kwa dhati.

Alisema Aga Khan iliamua kuanzisha kitivo cha hesabu na sayansi kuwaandaa walimu wazuri watakaoweza kufundisha mbinu za kujua hesabu.