Wanafunzi waliofaulu kidato cha kwanza lakini hawajui kusoma, kuandika kuchunguzwa

Saturday January 19 2019

By Yonathan Kossam, mwananchi [email protected]

Mbarali. Halmashauri ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya inakusudia kufanya uchunguzi juu ya madai ya kuwapo kwa wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu licha ya kuwa hawajui kusoma wala kuandika.

Madai hayo yameibuliwa na diwani wa Rujewa, Mkude Msasi katika kikao cha baraza hilo kilichofanyika leo katika ofisi za maji bonde la Rufiji wilayani humo.

Msasi amedai wapo wanafunzi wengi waliofaulu pasi kujua kusoma wala kuandika huku akieleza anao ushahidi wa wanafunzi hao.

"Mimi shuleni kwangu nina wanafunzi 536 lakini kuna wanafunzi zaidi ya mia na kitu hawajui kusoma wamechaguliwa wako pale," amesema Msasi.

Diwani huyo ameonyesha wasiwasi wake juu ya mfumo unaotumika kupima uwezo wa watoto kabla ya kujiunga na kidato cha kwanza na kuiomba Serikali kuliangalia jambo hilo kwa umakini zaidi.

Naye Diwani wa Mawindi, Mtaila Mhando ameiomba wizara ya elimu, sayansi na teknolojia kubadili mfumo wa utoaji maswali kwa kuondoa kabisa maswali ya kuchagua na kutia vivuli badala yake maswali yawe ni ya kujaza pamoja na kujieleza ili kuepuka udanganyifu kwa watoto wasiokuwa na uwezo darasani.

Advertisement

Mwenyekiti wa kamati ya elimu, Lwitiko Mwangosi amesema hawawezi kuyapuuza madai hayo hasa  ikizingatiwa diwani huyo amesema anao ushahidi juu ya uwapo wa tatizo hilo.

"Mkurugenzi hapa ananisikia ningeomba tushirikiane katika hili, kwani inawezekana mtoto alifaulu halali au alikopi," amesema Mwangosi

Mkurugenzi wa halamashauri ya wilaya ya Mbarali, Kivuma Msangi amesema tatizo hilo limewahi kujitokeza  ambapo watoto wanne walibainika hawajui kusoma wala kuandika na baada ya utafiti ilibainika wana uwezo kidogo wa kuandika na wengine hawana uwezo kuandika ila wa kunakiri tu.

Advertisement