Wanahabari: Uhuru wa habari nchini umezorota-VIDEO

Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzanua (TEF), Deodatus Balile

Muktasari:

Balile pia aligusia kufungiwa kwa magazeti mbalimbali, hatua inayochukuliwa na Idara ya Habari (Maelezo), akisema ni kinyume na Sheria ya Huduma za Habari (MSA, 2016) ambayo haimpi mamlaka hayo mkurugenzi wa idara hiyo.

Dodoma. Taasisi za habari nchini zimeeleza kuzorota kwa uhuru wa vyombo vya habari kutokana na matukio ya ukiukwaji wa haki za wanahabari na kutaka uwepo mjadala wa kitaifa.

Akisoma hotuba ya taasisi mbalimbali za habari katika maadhimisho ya 26 ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzanua (TEF), Deodatus Balile alisema kuna matukio mengi yaliyojitokeza mwaka huu ambayo yameathiri uhuru wa habari.

Hata hivyo, msemaji mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi akijibu tamko hilo kwa niaba ya Waziri wa Habari, Dk Harrison Mwakyembe, alisema Serikali inapendekeza kuundwa kamati ya kitaifa ya wataalamu kujadili changamoto katika sekta ya habari.

“Kama mkiwa tayari itaundwa hii kamati ambayo itachambua sheria zetu na changamoto nyingine katika tasnia ya habari na kuishauri Serikali ili hatua zilichukuliwe,” alisema Dk Abbasi.

Awali, Balile alisema taasisi kadhaa za habari zimekutana mara kadhaa kujadili uhuru wa vyombo vya habari kwa dhana pana ya uhuru wa wananchi kutoa mawazo yao. Balile alisema Aprili 9 hadi 13, TEF ilikutana jijini Tanga na kupitia hali ya uhuru wa vyombo vya habari Tanzania. Pia alisema, Aprili 24 Baraza la Habari Tanzania (MCT), lilichapisha taarifa ya Mwenendo wa Vyombo vya Habari na kubainisha upungufu.

“Familia ya waandishi wa habari tumesikitishwa na kauli ya Serikali Bungeni wiki iliyopita kuwa kuanzia sasa, watu wasiulizie suala la kupotea kwa mwandishi wa habari wa Gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda,” alisema Balile. Alisema tangu Novemba 23, 2017 hadi leo, mwandishi huyo wa habari wa kujitegemea hajulikani alipo, ikiwa zimepita siku 500.

“Kauli hii imeongeza hofu kwa waandishi wa habari hasa wale wanaoripoti habari za uchunguzi. Madai kwamba wamepotea watu wengi Kibiti, tunaamini kwa namna yoyote hayawezi kuhalalisha kupotea kwa Azory,” alisema Balile.

Alisema waandishi wa habari bado wanaiomba Serikali ifanye uchunguzi au iutangazie umma wa Watanzania hatua iliyofikia katika uchunguzi unaoendelea.

Balile pia aligusia kufungiwa kwa magazeti mbalimbali, hatua inayochukuliwa na Idara ya Habari (Maelezo), akisema ni kinyume na Sheria ya Huduma za Habari (MSA, 2016) ambayo haimpi mamlaka hayo mkurugenzi wa idara hiyo.

Alisema licha ya magazeti ya Mwanahalisi na Mawio kushinda kesi mahakamani, hadi sasa hayajapatiwa leseni na hivyo kushindwa kuendelea na uchapishaji huku akibainisha kuwa tangu mwaka 2016 hadi mwaka huu, Tanzania imeshuka nafasi 47 katika orodha ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani kati ya nchi 180.

Alisema sababu zinazotushusha ni sheria ikiwamo ya huduma za habari ya mwaka 2016, Sheria ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Takwimu na kanuni za maudhui za mwaka 2017.

Mbali na kueleza nia ya Serikali kuondoa changamoto katika sekta ya habari, Dk Abbasi aligusia madai ya matangazo ya Serikali kuzuiwa katika vyombo binafsi vya habari, akibainisha kuwa kwa sasa yamepungua lakini si kweli kwamba hayaendi.

Dk Abbasi alivitaka vyombo vya habari kuwa na ubunifu zaidi wa kuvutia wasomaji ili vipate matangazo kwani sasa ambao wanapata matangazo ni kutokana na jinsi chombo hicho kinavyosomwa. Wakizungumza katika maadhimisho hayo, Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Dk Inni Patterson walitaka uhuru wa habari kuendelezwa.

Cooke alisema Serikali ya Uingereza na taasisi zake ipo tayari kushirikiana na taasisi za habari nchini, kuhakikisha wanaboresha utendaji kazi na hivyo kuwa na uhuru wa upatikanaji habari za uhakika.

Maadhimisho mwa mwaka huu yameandaliwa na taasisi za MISA- Tanzania, TEF, MCT, Tamwa, UTPC, Mfuko wa Wakfu kwa Waandishi wa Habari (TMF), Sikika na Twaweza.