Wanakijiji wasimulia mkasa wa wazazi waliojiua Tabora

Adam Kalonga, Babu wa marehemu Amina Juma, akionyesha makaburi ya marehemu akiwa na Mwenyekiti wa kitongoji cha Gombe One, Gerson  Maganga (katikati) na jirani yao  Yona Mzava. Picha na Robert Kakwesi

Muktasari:

  • Ukosefu wa Sh2.6 milioni za tiba ya mtoto ndiyo chanzo

Tabora. Amina Juma na Kanuno Tano wanaweza kuwa wameondokana na machungu ya kumuona mtoto wao mdogo akiteseka kwa ugonjwa wakati hawana uwezo wa kifedha kwa ajili ya matibabu yake, lakini hatua yao ya kujiondoa uhai ni mwanzo wa matatizo makubwa zaidi kwa waliowaacha.

Amina (18), alitangulia kujitoa uhai kwa kunywa dawa tofauti baada ya kuona anashindwa kuvumilia kumuona mwanaye akiugua huku akishindwa kumudu fedha za matibabu na mumewe Tano (22), akajinyonga muda mfupi baadaye akisema hawezi kuishi bila ya mkewe.

Marehemu Amina na Tano walizikwa nyuma ya nyumba yao Aprili 6, 2019.

Vifo hivyo na sababu zake vimeacha simanzi na maswali mengi, huku wakazi wa Kijiji cha Kigombe wilayani Tabora wakitafakari hatua inayofuata kwa watoto wao wawili, mkubwa akiwa na umri wa miaka minne kutokana na hali yao ya kiuchumi kutokuwa nzuri.

Baadhi wanaona hatua ya wawili hao kujiua imetokana na msongo wa mawazo.

“Walikuwa na msongo wa mawazo uliotokana na kukosa zaidi ya Sh2.6 milioni zinazohitajika kwa ajili ya matibabu ya mtoto wao Chiku Kudona,” alisema Adam Kalonga, babu wa Amina wakati alipozungumza na Mwananchi jana.

“Walitakiwa wamrejeshe mtoto wao Hospitali ya (Rufaa) ya Bugando miezi miwili baada ye. Lakini sasa ni miezi mitano imepita.”

Walipokwenda mara ya kwanza kwa ajili ya matibabu ya mtoto wao, wawili hao walitumia zaidi ya Sh320, 000.

“Kukosa fedha za matibabu huku mtoto akiendelea kutaabika kwa maradhi kuliwaumiza Amina na mumewe Tano. Mara kwa mara Amina alikuwa akilia kila alipomwangalia mtoto wake mgonjwa anavyoteseka,” alisema Kalonga.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Gombe One, Gerson Maganga alisikitika kwa jinsi ambavyo kijiji kilishindwa kuchukua hatua baada ya wawili hao kutoa taarifa ya matibabu ya awali na mahitaji yaliyotakiwa kwa ajili ya kurudi Hospitali ya Bugando kwa matibabu zaidi.

“Waliporejea kutoka Hospitali ya Bugando, waliujulisha uongozi wa kitongoji mahitaji ya fedha kwa ajili ya matibabu ya mtoto wao, lakini kwa bahati mbaya hawakusaidiwa,” alisema Maganga.

“Hatukujua kama hali ingefikia hapo ilipofika. Tunaomba Mungu atusamehe kwa kushindwa kufanya jambo ambalo pengine lingeokoa maisha ya wanandoa hawa walioamua kujitoa uhai kutokana na ugonjwa wa mtoto wao.

“Tunawaomba Wasamaria wema wajitokeze kusaida matibabu ya mtoto huyu.”

Kuhusu maisha yao, Maganga alisema enzi za uhai wao, ndoa ya Amina na Tano ilikuwa mfano wa kuigwa kwa jinsi walivyoishi kwa amani na ushikirikiano katika kila jambo.

“Wamedumu kwenye ndoa kwa miaka mitano pekee na walikuwa vijana wadogo, lakini walikuwa miongoni mwa familia za mfano katika kitongoji chetu,” alisema Maganga.

Lakini kazi inayowasubiri ndugu, jamaa na wakazi wengine wa kijiji hicho ni malezi ya watoto hao wawili na matibabu ya Chiku.

Akizungumzia malezi ya watoto hao yatima, Chiku Shaaban ambaye ni mama mzazi wa Amina, aliwaomba wasamaria wema kujitokeza kumsaidia kuwalea na kuwahudumia.

“Tutakuwa na wakati mgumu kuwalea na kuwatunza watoto hawa kutokana na umri wao na ugonjwa wa mtoto mdogo. Tukisaidiwa tutashukuru Mungu,” alisema Chiku.