Wananchi hawajaamua 2015: Asilimia 42 hawana mgombea wanayemtaka

Saturday November 15 2014Takwimu katika picha

Takwimu katika picha 

By Waandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Ripoti ya utafiti iliyotolewa katikati ya wiki hii na Taasisi ya Twaweza ikuhusu maoni na matakwa ya wananchi kuhusu uongozi wa kisiasa, imeonyesha kuwa asilimia kubwa ya Watanzania bado hawajaamua nani wampigie kura au chama gani wakiweke madarakani katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani.

Hali hiyo inavipa nafasi vyama vya siasa kufikiri na kupanga upya mikakati yake, kwani asilimia zilizoonyeshwa kuwa ndiyo kura watakazopata wagombea watarajiwa kama uchaguzi ungefanyika leo, zinaonyesha kwamba kiwango cha kukubalika cha wagombea wote wa CCM na hata wa upinzani bado ni kidogo.

Hii ni kuonyesha kuwa kuna asilimia 42 ya watu ambao mpaka sasa hawajaamua watamchagua nani kati ya wale wanaotajwa kuwa huenda wakagombea urais, kati ya hao asilimia 33 ni wale waliosema hawajui wamchague nani, asilimia nane ni wale waliosema watawachagua wagombea wengine watakaojitokeza (ambao hawajatajwa wala hawatambuliki kwa sasa) na asilimia moja ni wale waliosema hawana mtu yeyote wa kumchagua.

CCM yaongoza

Ingawa utafiti unaonyesha kuwa CCM imepewa nafasi kubwa ya kuongoza kama uchaguzi utafanyika leo, lakini uongozi wake siyo wa kukifanya chama hicho kilale usingizi mnono, kwani takwimu zinaonyesha kuwa mwaka hadi mwaka mapenzi ya chama yanapungua na hivyo hivyo matakwa ya wapigakura.

Katika uchaguzi wa mwaka 2000 CCM ilipata asilimia 71 ya kura zilizopigwa, mwaka 2005 ilipata 76, lakini mwaka 2010 ilishuka hadi 53 na kama Watanzania wangelipiga kura mwaka huu CCM ingepata asilimia 54 ya kura zote.

Advertisement

Hata hali hiyo bado haiipi faraja CCM kwa sababu ni wazi kuwa kura itakazopata kwa kiasi kikubwa itategemea mgombea atakayesimamishwa.

Hawa wanaotajwa hivi sasa ama wamejitangaza au hawajajitangaza, hakuna aliyepata kukubalika kwa asilimia kubwa kutoka mwaka 2012, Twaweza ilipoanza kufanya utafiti wake.

Kwa mujibu wa utafiti huo, mapendekezo ya wana CCM kuhusu rais wanayemwona anafaa yalikuwa kama ifuatavyo: Mwaka 2012, Edward Lowassa alipata asilimia nane, 2013 (20) na 2014 (17).

Mizengo Pinda mwaka 2012 alipata 23, 2013 na 2014 alipata asilimia 14 ya wananchi waliotoa maoni yao kura kwa njia ya simu.

John Magufuli mwaka 2012 alipata asilimia 8, 2013 (6) na 2014 (5). Hivyo inaonyesha kuwa imani ya wapenzi wa chama husika juu ya wagombea wao watarajiwa inashuka kila mwaka.

Watakaompigia kura mgombea yeyote wa chama chao

Pamoja na hayo, lipo kundi la watu ambao wako tayari kumpigia kura mgombea yeyote atakayechaguliwa na chama chao, hawa ni asilimia 24 ya waliohojiwa.

Hawa inaonyesha kuwa hawana chaguo, hivyo ni rahisi kurubuniwa. Lakini lipo pia kundi jingine la watu ambao hawajui chochote na hawana uhakika, hawa ni asilimia 18.

Hii ni asilimia kubwa kitakwimu ambayo jitihada za kuwaelimisha zisipochukuliwa ipasavyo, hizi ni kura zisizojitambua, hivyo zihesabike kama ni kura za kupotea.

Kwa mujibu wa utafiti huu, mwaka 2015 CCM ina kazi kubwa ya kufanya ili kujiweka katika nafasi ya ushindi wa kupendeza, ushindi wa kishindo. Kinyume cha hivyo itaburuzwa na vyama vya upinzani hasa katika maeneo ya mijini katika mikoa ambayo upinzani umejizatiti.

Umri

Kadhalika lipo suala la upenzi wa chama kwa makundi ya umri, utafiti umeonyesha kuwa CCM inapendwa na watu umri wa kati ya miaka 35 na zaidi ya 50 wakati Chadema kinapendwa na vijana wa chini ya miaka 35.

Takwimu hizo zina maana mbili: Kwanza; CCM inayoyoma na wazee, hivyo ina kazi ya kuwashawishi vijana zaidi kukipenda na kujiunga na chama hicho.

Pili; Chadema ina wapenzi na wafuasi wengi vijana, hawa ni watu ambao ni rahisi kubadilika kimsimamo na kimtazamo, inategemea tu na ushawishi uliopo kwa wakati husika. Hivyo Chadema nayo inapaswa kufanya jitihada ya kutafuta mapenzi na ufuasi wa watu wazima ili chama kisiyumbishwe na upepo.

Ingawa utafiti huu haukuishirikisha Zanzibar, ukiangalia nafasi ya CUF Bara, utaona ni sawa na hakuna. Kati ya watu 2,000 walioulizwa chama wanachopendelea asilimia saba hadi 12 walisema kuwa hawana chama na asilimia sita hadi nane walisema wanapendelea chama cha upinzani kisichokuwa Chadema, lakini hawajaipa CUF kipaumbele kikubwa.

Katika nafasi za ugombea urais, kama kura zingepigwa sasa CCM ingepata asilimia 51, Chadema (23), CUF ingepata asilimia nne tu.

Hapo hapo lipo kundi la watu 16 waliosema kuwa wanapigia mgombea siyo chama. Hawa asilimia 16 wanaonyesha kuwa mgombea binafsi pia ana nafasi katika uchaguzi wa mwakani.

Wasiojua wampigie kura nani waongezeka

Pia ripoti hiyo inaonyesha kuwa idadi ya wananchi wasiojua wampigie kura mgombea wa chama gani imeongezeka tangu 2012 kutoka asilimia 22 hadi 33 mwaka huu.

Mwaka 2012 wananchi asilimia 15 walitaka wajitokeze wagombea wengine ndipo waweze kumchagua mmoja wao kuwania kiti cha urais. Katibu Mkuu wa Chadema, Willibrod Slaa ndiye aliyeonekana kupendwa zaidi kwa kupata asilimia 19, akifuatiwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa asilimia 16, kwa mwaka huo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliambualia asilimia sita.

Hata hivyo, Ripoti inaonyesha kuwa mwaka uliofuata Lowassa alipanda hadi kufikia asilimia 13, huku Dk Slaa akibakia kwenye asilimia 19 hadi alipoporomoka mwaka huu kwa kupata asilimia 11.

Waliopanda na kushuka

Matokeo ya utafiti huu huenda yasiwafurahishe baadhi ya wagombea baada ya kuonyesha wakizidi kuporomoka kila mwaka, huku yakiwapa nguvu baadhi yao.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, takwimu zinaonyesha kuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba amekuwa akipanda kila mwaka kutoka asilimia tatu 2012, asilimia tano 2013 hadi asilimia sita mwaka huu.

Mwingine anayeonekana kufanya vizuri ni aliyekuwa Spika wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, ambaye amepanda kutoka asilimia mbili 2012, asilimia tatu 2013 hadi asilimia nne 2014.

Walioporomoka katika orodha hiyo ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli ambaye 2012 alipata asilimia sita, 2013 asilimia tano na mwaka huu amenyakua asilimia tatu.

Pia Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ameporomoka kutoka asilimia tatu 2012 na mwaka jana hadi asilimia moja 2014.

Mchuano mkali CCM

Wakati wanasiasa ndani ya CCM wakipigana vikumbo kutaka kuteuliwa kupeperusha bendera ya urais kwa tiketi ya chama hicho, matokeo ya utafiti yanaonyesha mvutano mkali huku idadi ya wasio na uhakika wamchague nani ikizidi kushuka.

Takwimu zinaonyesha kuwa Lowassa anaongoza kwa asilimia 17 akiporomoka kutoka asilimia 20 alizokuwa amepata mwaka jana. Pinda ndiye anayefuata akiwa na asilimia 14, pia akiwa ameporomoka kutoka asilimia 23 alizozipata 2012.

Ripoti inasema kuwa ushindani mkubwa unatokana na wananchi wengi ambao wanasema watamchagua yeyote atakayepitishwa na chama.

“Sehemu kubwa (24) imekwenda kwa ‘mtu yeyote atakayeteuliwa na CCM,” inasema ripoti hiyo.

Asilimia 18 wanasema hawajui wamchague mgombea gani wa CCM huku asilimia 10 wanataka mgombea mwingine ambaye bado hajajitokeza.

Nafuu kwa Ukawa

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wananchi wanne kati ya 10 (41) walimtaja Dk Slaa kuwa ndiye anayefaa kupeperusha bendera ya urais kupitia Umoja wa Katiba wa Wananchi (Ukawa).

Majina mengine ya viongozi wa upinzani yaliyopata zaidi ya asilimia 10 ni Lipumba (14) na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe asilimia 11.

Wengine ni Zitto Kabwe asilimia sita, Maalim Seif Sharif Hamad, James Mbatia na Augustino Mrema wote asilimia moja kila mmoja. Hata hivyo, zaidi ya asilimia 21 walisema hawajui wampigie kura nani.

Kaduma

Mwanasiasa mkongwe nchini, Ibrahimu Kaduma alisema jambo la msingi kwa sasa ni kila Mtanzania kumwomba Mungu atupe kiongozi mzuri, badala ya kuegemea kwenye takwimu na tafiti.

“Mungu anajua kiongozi gani anakula rushwa, atatupa mtu atakayeweka masilahi ya taifa mbele. Sisi tunatafuta kiongozi atakaye tutumikia na siyo atakaye jitumikia… Kiongozi mzuri anaweza kutoka chama chochote,” alisema Kaduma.

Mwenyekiti wa CCM Iringa, Jesca Msambatavangu alisema wananchi wengi bado hawajaamua mtu wanayetaka awe rais wao kwa sababu hawajapewa taarifa za kutosha.

“Mara nyingi uchaguzi unapokaribia wananchi ‘wanaamshwa’ kwa kuwa ni wachache tu wanaojishughulisha na mambo ya siasa. Kwa hiyo inategemea na aliyefanya utafiti amekwenda wapi,” alisema Jesca.

Aliongeza: “Huwezi kwenda kwenye makundi ya watu na kuwauliza ‘mnataka nani awe rais?’ wanakwambia wanasubiri yeyote atakaye jitokeza.”

Mwenyekiti huyo ambaye pia ametangaza kugombea ubunge kwenye Jimbo la Iringa Mjini mwakani, alisema watu wengi hawajajitokeza kutangaza nia kwa sababu wakati sahihi wakufanya hivyo haujawadia.

Utafiti huu wa Twaweza kwa kiasi kikubwa umejaribu kuonyesha hisia za wananchi.

Hivyo wanasiasa wanapaswa kuufanyia kazi na si kuubeza. Kama wanavyosema wanasiasa kuwa upepo wa kisiasa ni vigumu kuutabiri, kwani wakati wowote huweza kubadili mwelekeo.

Imeandikwa na Hawra Shamte na Goodluck Eliona.

Advertisement