Wananchi walivyozungumzia kauli ya Jaguar

Wednesday June 26 2019

 

By Mwandishi wetu, Mwananchi

Licha ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kuwatuliza Watanzania kuhusu kauli ya mbunge wa Sterehe, Charles Njagua Kanyi maarufu Jaguar aliyewapa saa 24 raia wa kigeni nchini humo kuondoka ikiwemo Watanzania, mbunge huyo ameendelea kushambuliwa mitandaoni.

Jana Jumanne Kuni 25, 2019 Majaliwa alitoa kauli ya Serikali Bungeni kuhusu suala hilo la Jaguar akisema Serikali ya Kenya imemkana mbunge wa nchi hiyo, na imemtaka aeleze alitoa kauli hiyo akiwa analenga nini.

Kupitia mitandao ya kijamii ya Mwananchi yaani Facebook, Twiter na Instagram Watanzania wameendelea kumshambulia mbunge huyo na kumtaka aombe radhi kuthibitisha alikosea kutoa kauli hiyo.

Hata hivyo, tayari vyombo vya dola nchini Kenya wamemkamata mbunge huyo kwa mahojiano kuhusu kauli hiyo.

Katika akaunti ya Instagram Brightontewele ameandika, “Alikuwa na maana gani? Si alimaanisha watanzania watoke kesgo la sivyo atahamasisha wapigwe hadi mamlaka ya uhamiaji iwapeleke Airport, atoke hadharani aombe radhi,”

“Wamemchukulia hatua gani mpaka sasa sio tu kusema sio msimamo wa serikali ya Kenya, hiyo haitoshi,” amesema Allysaidmngagi huku Paul David akisema, “Ni kumsamehe tu kwa kauli zake tata, kuna muda binaadam anajisahau kama ilivyo baadhi ya kauli za viongozi vijana hapa kwetu, Kenya ni ndugu zetu.”

Advertisement

Ha Saningo ameandika, “Hawa watoto hawajui kabisa wazee wetu Kenyata, Nyerere, Obote walitumia muda wao kutufanya tuwe ndugu Kenya ,Uganda, Tanzania leo wanaropoka na kuleta ubaguzi hadharani.”

Christopher Mwakaje amesema, “Bado naamini ni kuropoka Kwa Jaguar tu japokuwa ni lazima akemewe ipasavyo.” Huku Izack Kipruto amesema kauli kama hizo sio zakipuuza.

Advertisement