VIDEO: Wananchi wataka bajeti 2019/2020 kugusa maisha yao, wengine hawajui lolote

Wednesday June 12 2019

bajeti kuu , Serikali  Tanzania, bunge Dodoma, Waziri wabunge, Upinzani ,Vyama siasa, CCM,

 

Dar es Salaam. Wakati bajeti kuu ya Serikali ya Tanzania mwaka 2019/2020 ikitarajiwa kusomwa bungeni kesho Alhamisi Juni 12, 2019, wananchi wametoa maoni tofauti  huku baadhi wakitaka iguse maisha yao na wengine wakisema hawajui lolote.

“Unajua nini kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali”, ndio swali lililoulizwa katika mitandao ya kijamii ya Mwananchi, kujibiwa na baadhi ya wasomaji wakitaka kuona bajeti hiyo ikiondoa changamoto za maisha yao.

Andwele Lugano amesema, “Bajeti inatakiwa kugusa maisha ya watu kwa kuwaondolea changamoto zao za maisha, hatutaki bajeti za kwenye vyombo vya habari kutwa kusifiana tu wakati watu bado wana changamoto kibao.”

Kwa upande wake Manka Swai amesema,  “Badala niwaze life (maisha) yangu eti nawaza bajeti inanisaidia nini mimi nipo shamba huku napambana na ngedere wasimalize mazao yangu niliolima kwa jasho.”

Nicksoni Chilale amesema yupo gizani kuhusu bajeti hiyo kwa sababu televisheni hazionyeshi matangazo ya Bunge ya moja kwa moja.

Msomaji mwingine, Denis Stephano amesema anachofahamu bajeti ni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha katika kipindi fulani ili kuhakikisha mipango inafanikiwa kwa wakati uliotarajiwa.

Advertisement

Mwingine aanayejiita Mtanzania amesema bajeti ni kiini macho kwa madai kuwa kile kinachodaiwa kinapelekwa ni kidogo kuliko kilichokusudiwa.

“Bajeti yetu kwa asilimia kubwa inategemea fedha zetu za ndani hivyo kuifanya isikidhi haja na ndio sababu wanaanzisha kodi za ajabu ili angalau kufikia nusu ya bajeti lakini kwa sababu fedha tunazokosa kutoka kwa wahisani ni nyingi bado inaonekana bajeti hiyo kutokidhi haja, mwambieni mkuu wa nchi abadili mfumo kinyume chake twafa,” amesema Mtanzania.

Kwa upande wake Mary Kagose amesema, “Najua watumishi hawaongezewi salary (mshahara) na wananchi watalimia meno.”

Rogers Sikawa amesema, “Ninafahamu ni bajeti ya maisha bora kwa viongozi wakuu na familia zao.”

Naye Lucy Stephen amesema, “Nafahamu kila mwaka huwa ni bajeti ya tarakimu isiyotekelezeka, na ambayo haigusi maisha ya Mtanzania wa kawaida kabisa? Mengine naogopa kuandika kuhofia wasiojulikana!”

Richard Masanja amesema, “Hatima ya Watanzania wote ni kesho nafikiri kilio kitaendelea maana Serikali hii sio rafiki kwa wanyonge.”

Baba Wardah Mhandeni amesema, “Ninajua bajeti hiyo vema tu, sifa yake kubwa ni wizara kuahidiwa na kupitishiwa mabilioni ya fedha kisha huishia kupata milioni 50 tena kwa mbinde.”


Advertisement