Wananchi wazungumzia msuguano wa Spika Ndugai, Profesa Assad

Monday April 15 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kauli ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad kwenda kujieleza kwa Rais John Magufuli, imepokelewa kwa mtazamo tofauti na wananchi huku wakieleza inalenga kuzima mjadala kuhusu taarifa ya hesabu iliyotolewa.

Jana Jumapili akiwa katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Spika Ndugai alimtaka Profesa Assad akajieleze kwa Rais Magufuli kwani anampa wakati mgumu, pia alimshauri kumaliza mgogoro kati yake na Bunge kwa kwenda kwa Rais kumwambia alikosea.

Hata hivyo, Profesa Assad amesema Katiba ya Jamhuri ya Muungano haina kifungu kinachomtaka akajieleze.

Katika mitandao ya Mwananchi ya Twitter, Instagram na Facebook wananchi wametoa maoni tofauti tofauti juu kauli ya Spika Ndugai na Profesa Assad.

Hence Mruma ameandika, “Jadilini ripoti ya CAG, kwani kuna shida gani, neno dhaifu kwa wakaguzi ni kawaida kutumiwa sidhani kama CAG ana kosa labda mkabadili matumizi ya neno hilo kwa wakaguzi. Unapofanya evaluation na systeam ukakuta ina matatizo basi kwenye ripoti unasema systeam ni dhaifu.”

Wakati huyo akisema hivyo bizzshopjoh ameandika, “Mimi ningekuwa Rais ningelifuta Bunge, maana Bunge lililopewa jukumu la kuisimamia Serikali wanaanzisha migongano na waliowapa kazi, sisi wananchi hatupendezwi na namna linavyofanya kazi kwa sasa.”

Naye Robert Nicholaus akaandika, “Kwani Rais ndiye aliyemkataa mbona Bunge linakuwa na wasiwasi na maamuzi yake kama liliamua kwa busara inatosha. Kila kitu kigumu mnapeleka kwa Rais, madaraka ya Bunge yako wapi?,”

Dk of Gems ameandika, “Kwa hiyo Ndugai hajui CAG ashatoka kwa Magufuli kumpa ripoti ndio akaipeleka bungeni.”

Mapala Mapala ameandika, “Profesa Assad anazidi kutufundisha kwamba kila mtu ataishi na kufanya kazi kwa mujibu wa katiba na sheria basi hapo hatutakuwa na ugomvi wala mikwaruzano.”

Igwe ameandika, “Spika ndo ajiuzulu maana anatupa wakati mgumu sisi wananchi.” Saidimwalukope yeye amesema, “Prof Mussa Assad ndio tunu ya watanzania kwa sasa.”

Noel Shao anasema, “Kimsingi kumuondoa Spika ni rahisi kuliko kumuondoa CAG. Hata Katiba ina loophole kubwa ya kumtoa Spika kuliko CAG. Sasa hoja ni kuwa ni nani aliyepwaya anayepaswa kuondolewa? Hili ndilo swali la msingi la kuweka kwenye mzani.”

Raheem Saleh ameandika, “Mwanasiasa bhana akikutana na msomi na mfata haki (real) huwa wanapagawa, inatakiwa tupate CAG kama hawa ata 10 tu wanasiasa wasingesumbua saana.”

Kwa upande wake, Lucas Chambalo amesema, “CAG, Mimi nadiriki kuamini wewe ni Chaguo la Mungu, maana umesimamia haki na kweli. Na ukweli siku zote utakuweka huru, Mungu akulinde na mabaya yote Ameen.”

Advertisement