Wanasheria wasema Lissu anaweza kuhojiwa popote alipo

Muktasari:

Wakati Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola akilishangaa Jeshi la Polisi kutomkamata Tundu Lissu hadi sasa, wanasheria nchini wamesema mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema) anaweza kuhojiwa popote alipo

Dar es Salaam. Wakati Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola akilishangaa Jeshi la Polisi kutomkamata Tundu Lissu hadi sasa, wanasheria nchini wamesema mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema) anaweza kuhojiwa popote alipo.

Leo Alhamisi Februari 14, 2019 Lissu amefikisha siku 524 tangu apigwe risasi jijini Dodoma, na jana Lugola katika mkutano wake na wanahabari alishangazwa na polisi  kushindwa kumkamata mwanasheria mkuu huyo wa Chadema.

Wanasheria hao wamesema sheria na utaratibu wa jeshi hilo unaliwezesha kuendelea na uchunguzi hata kama mbunge huyo yuko nje ya nchi.

Lugola pia alitumia mkutano huo kujibu hoja za Lissu alizozitoa Marekani anakofanya ziara kuzungumzia tukio la kushambuliwa kwake pamoja na masuala ya siasa na utawala bora nchini.

“Kama amepata nafuu (Lissu) badala ya kuanza uzembe za uzururaji alipaswa kuja (nchini). Nashangaa polisi kila siku wanahangaika kukamata vijana kwa uzururaji na kumuacha huyu (Lissu),” amesema Lugola.

Lissu alishambuliwa mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake Area D, jijini Dodoma wakati akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge akiwa na dereva wake Adam Bakari ambaye hakujeruhiwa.

Alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali na siku hiyohiyo usiku alihamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Alipata matibabu katika hospitali hiyo hadi Januari 6, mwaka jana alipohamishiwa Ubelgiji.

Desemba 31, 2018 aliruhusiwa kutoka hospitali huku akieleza kuwa amepewa ruhusa licha ya kuwa bado yupo katika matibabu na akaanza ziara Ulaya na Marekani.

Walichokisema wanasheria

Mwanasheria wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Paul Mikongoti ameitaja Sheria ya Kusaidiana kwenye mambo ya jinai (Mutual assistance in criminal matters) akisema ndiyo inayoliongoza Jeshi la Polisi kwenda kuhoji wahalifu au waathirika wa matukio ya jinai wakiwa nje ya nchi.

“Sheria zipo zinazoliwezesha Jeshi la Polisi kumhoji Lissu. Hata wao Polisi wenyewe wanaweza kwenda kwa kushirikiana na majeshi ya Polisi kama ya Kenya au Ubeligiji au mtandao wa Polisi wa kimataifa (Interpol),” amesema Mikongoti.

 Amesema Serikali inaweza kutumia ofisi za ubalozi kumhoji Lissu na dereva wake tangu alipokuwa nchini Kenya na Ubeligiji.

“Tuna ubalozi Kenya, tuna ubalozi Ubeligiji wangeweza kutuma maofisa wao kwenda kumhoji. Sijui kwa nini hawajamhoji, wao wenyewe wanajua, lakini kuna sheria inayoitwa Mutual assistance in criminal matters, inayotoa mwongozo wa kwenda kuhoji watu kama hao,” amesema.

Mmoja wa mawakili ambaye hakutaka jina lake kuwekwa wazi amesema Jeshi la Polisi halina sababu ya msingi la kushindwa kumhoji Lissu popote alipo duniani.

“Issue (suala) si sheria, Jeshi la Polisi linapotakiwa kumhoji mtu, kama nje ya nchi na hasa alipokuwa Kenya alipopata fahamu wangekwemda kumhoji. Kwa hiyo wanaweza kumhoji mahali popote hakuna kitu chochote kinachozuia kwenda kumhoji,” alisema wakili huyo.

“Hata kama mtu ni shahidi muhimu na yuko nje ya nchi na imekuwa ngumu kumleta, Jeshi la Polisi linakwenda kumhoji. Sioni kama ni defence kwamba hajahojiwa,” amesema.

Amesema Jeshi la Polisi katika upelelezi linaweza kwenda popote, hata kama ni Marekani.

“Ni ngumu kutetea kwamba Jeshi la Polisi limeshindwa kuendelea na upelelezi kwa sababu halikwenda kumhoji, haiingii akilini,” alisisitiza wakili huyo.

Wakili mwingine kwa sharti la kutotajwa jina amesema pia ameitaja  sheria hiyo ya kusaidiana katika masuala ya jinai.

“Kifungu cha 14(1)(b)(ii) kinaeleza bayana, unapokuwa Tanzania kuna uchunguzi wa jinai unafanyika, halafu kuna mtu mwenye ushahidi muhimu lakini hayupo Tanzania, Mwanasheria mkuu akiona ushahidi muhimu anachukua mamlaka ya kuwasiliana na nchi nyingine ili wachukue ushahidi kule aliko mtu,” amesema wakili huyo.

“Iwe Kenya iwe Ubelgiji, yaani kwa hali ya kawaida, mgonjwa alazwe Uingereza halafu muache kuchunguza ugaidi?” Alihoji.

Ametaja pia mabadiliko ya sheria ya ushahidi ya 2017 yalifanyika ili kuendana na kasi ya teknolojia akisema mtuhumiwa au mwathirika anaweza kuhojiwa popote alipo duniani kwa njia za mawasiliano ya elektroniki.

“Mabadiliko hayo yaliyotanguliwa na mahakama za juu nchini, Polisi wanaweza kuhoji mtu akiwa nje ya nchi. Wewe ni askari wa upelelezi unaweza kuyarekodi maelezo yenu kwa njia ya video, si unamwona kule kule anatoa ushahidi? Kwa nini ishindikane kumhoji mtu aliye Nairobi au Ubeligiji?” Amehoji.

Amesema njia ya tatu ya kutuma watu alipo mwathirika wa tukio ili kumhoji akisema pia inawezekana.

“Haiwezekani maisha yakasimama 2019 eti kwa sababu mtu hayupo nchini,” amesisitiza.