Wanawake wenye nia ya kuwania uongozi waanza kupikwa

Muktasari:

Wanawake wenye nia ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2020 wameanza kujengewa uwezo wa namna ya kushiriki na kushinda


Dar es Salaam. Wanawake wenye nia ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2020 wameanza kujengewa uwezo wa namna ya kushiriki na kushinda.

Akizungumza katika mdahalo wa ushiriki wa wanawake kwenye uongozi ulioandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), mkurugenzi wa mtandao huo, Lilian Liundi amesema ili kufikia usawa wa kijinsia kwenye uongozi, wanawake wenye nia ya kuingia madarakani lazima wajengewe uwezo.

Amesema mtandao huo unacho chuo cha mafunzo ya kuwapika na kuwanoa viongozi mbalimbali wakiwamo wanaotaka kuwania ubunge, udiwani na nafasi kubwa zaidi.

“Sio tu uongozi kwenye ngazi za kisiasa hata kwenye taasisi na mashirika bado wanawake tunatakiwa kushiriki kwa kiwango kikubwa,” amesema.

Mbali na mafunzo, Liundi amesema wataanzisha utaratibu wa viongozi wanawake wazoefu kuwashika mkono wenzao ili kuwavuta kwenye nafasi hizo wakiwapa uzoefu wa namna wao walivyofanikiwa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Victoria Lihiru amesema kutokana na hali ya kisiasa ilivyo kuna haja ya wanawake kuandaliwa mpango wa mafunzo mapema ili kuwanoa waweze kushindana kisiasa.

“Inaonekana hali ya kisiasa itakuwa ngumu na huenda hali hiyo ikasababisha wanawake kutogombea kwa hiyo lazima kuwajengea uwezo,” amesema.

Awali,  mbunge wa viti maalum, Ester Mmasi amesema jambo la muhimu kwa wanawake wanaotaka kuwania nafasi za uongozi ni kuitambua na kuifanyia kazi nia hiyo kwa kuchukua hatua.

“Hata ukishikwa mkono kama ndani yako hakuna hiyo spirit (nia) haitasaidia kitu kwanza uwe na nia halafu ingia kugombea bila kusuasua hapo ni rahisi kupenya,” amesema.

Akifungua mdahalo huo, ofisa wa ubalozi wa Finland nchini, Elina Kalikku amewashauri wanawake kuwa na mtandao wenye nguvu utakao wawezesha kuwa na sauti moja katika harakati za kupata usawa kwenye uongozi.

“Ili uwe kiongozi mzuri lazima ujifunze kuwa kiongozi mzuri, Finland tulishawahi kuwa na Rais mwanamke,  waziri mkuu na mawaziri wengine na nchini kwetu tulianza masuala ya harakati hizi mwaka 1906 tukianza na wabunge 19,” amesema.