Wanigeria wawili mbaroni tuhuma dawa za kulevya

Muktasari:

  • Raia wawili wa Nigeria wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin kilogramu 15.8

Dar Es Salaam. Raia wawili wa Nigeria akiwamo anayejiita mchungaji  wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilogramu 15.8.

Washtakiwa hao, Henry Ogwuanyi (44)  ambaye anajiita anajitambulisha kama mchungaji na Onyebuchi Ogbu (34) wote ni wafanyabiashara na raia wa Nigeria.

Wakili wa Serikali, Constantine Kakulaba amedai mahakamani hapo leo Aprili 24  kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 34/ 2019.

Aksoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi,  Kakua  alisema washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la kukutwa na dawa  za kulevya kinyume cha sheria.

Kakula alisema washtakiwa hao walitenda kosa hilo April 2 mwaka huu  katika eneo la Msimbazi, wilaya Ilala.

Alidai siku hiyo ya tukio, Ogwuanyi na Ogbu walikutwa na dawa za kulevya aina ya heroin kilogramu 15.8 kinyume cha sheria.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, Hakimu Shaidi alisema washtakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote kutokana na Mahakama ya Kisutu kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa Mahakama Kuu au kwa kibali maalumu.

Kakula alieleza kuwa upelelezi wa shauri hilo  haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 8 mwaka huu itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana.