Wapewa mizinga ya nyuki kutunza mazingira

Muktasari:

Akizungumza na Mwananchi jana, mratibu mradi wa Kisiki Hai wilaya ya Mpwapwa, Emmanuel Majele alisema mizinga hiyo imetolewa na shirika la Lead Foundation.

Mpwapwa.Wakazi wa wilaya za Kongwa na Mpwapwa mkoani Dodoma wamepatiwa mizinga 60 ya nyuki kwa lengo la kutunza mazingira na kujipatia kipato.

Akizungumza na Mwananchi jana, mratibu mradi wa Kisiki Hai wilaya ya Mpwapwa, Emmanuel Majele alisema mizinga hiyo imetolewa na shirika la Lead Foundation.

“Tumeamua kutoa mizinga hiyo ya nyuki kwa wanakijiji ili kutunza mazingira katika milima ya Kiboriani ambayo ndiyo chanzo kikubwa cha maji katika wilaya za Kongwa na Mpwapwa,” alisema.

Alisema mradi wa Kisiki Hai unawakataza wananchi kung’oa visiki wakati wa kuandaa mashamba yao kwenye msimu wa kilimo, hivyo wameona ni vyema kuwapa mizinga ya nyuki kwa ajili ya kujishughulisha na ufugaji huo.

Mkazi wa kijiji cha Kiboriani wilayani Mpwapwa, Erick Chizua alisema mradi huo umewanufaisha hasa katika kipindi cha kiangazi shughuli za kilimo zinaposimama wanakuwa wanajishughulisha na ufugaji nyuki ambao hauna gharama kubwa.