Wapinzani wadai ushindi wao Congo

Wednesday January 9 2019

Kinshasa, DRC. Timu ya Kampeni ya mgombea urais nchini Congo Felix Tshisekedi, imesema wawakilishi wa kambi yao wamekutakana na kambi ya rais anayemaliza muda wake Joseph Kabila kuhakikisha makabidhiano ya amani ya madaraka.

Kambi ya Kabila hata hivyo imekanusha kuwepo na mikutano kama hiyo tangu kufanyika kwa uchaguzi wa Desemba 30, ambao matokeo yake ya awali yanatarajiwa kutangazwa wiki hii.

Uchaguzi huo ulitarajiwa  kuleta mabadiliko ya kwanza ya Kidemokrasia nchini Congo katika kipindi cha miaka 59 ya uhuru wake, lakini wasiwasi unazidi kuenea huku baadhi ya wanasiasa wa upinzani wakiituhumu Serikali kutaka  kuiba kura.

Matokeo  yanayobishaniwa huenda yakazusha aina ya vurugu zilizoshuhudiwa baada ya uchaguzi wa mwaka 2006 na 2011 na kuvuruga tena usalama katika maeneo ya mpakani mwa DRC na Uganda, Rwanda na Burundi.

Tshisekedi aligombea urais akiwa mgombea aliyeteuliwa na kabila mwenyewe Emmanuel  Shadary, na kiongozi mwingine wa upinzani Martin Fayulu, ambaye uchunguzi wa maoni ya wapigakura kabla ya uchaguzi ulimuonyesha akiongoza kinyang’anyiro hicho.

Wafuasi wa Fayulu

 

Ripoti za mawasiliano kati ya kambi za Tshisekedi na Kabila zimewapa wasiwasi baadhi ya wafuasi wa Fayulu wakihofia kwamba huenda Kabila anajaribu kujadili ugawanaji wa madaraka na Tshisekedi.

Kwenye mkutano na waandishi habari, Katibu Mkuu wa chama cha siasa cha Tshisekedi cha UDPS, amesema mawasiliano kati ya kambi mbili yalikuwa yanachangia maridhiano ya kitaifa, na kwamba chama cha UDPS kinapinga sera yoyote ya kulipiza vizazi.

 

"Watu hao wawili (Kabila na Tshisekedi) wana maslahi katika kukutana kuandaa mazingira ya amani na ya ustaarabu ya kukabidhiana madaraka," Jean-Marc Kabund alisema.

Msemaji wa Tshisekedi, Vidiye Tshimanga, baadae alisema Kabila na Tshisekedi hawajakutana ana kwa ana tangu uchaguzi lakini kwamba wawakilishi wake wamekutana mara kadhaa.

 

Kambi ya Kabila yakana

 

Mmoja wa washauri wa Kabila na msemaji wa Shadary, Barnabe Karubi ,alikanusha kwamba kulikuwepo na mawasiliano yoyote na Tshisekedi au wawakilishi wake.

Kwenye mkutano wake na waandishi habari siku ya Jumanne, muungano wa vyama tawala umeituhumu kampeni ya Fayulu na maaskofu wa Congo kwa kujaribu kuchochea vurugu za baada ya uchaguzi katika taifa hilo kubwa lenye utajiri wa madini.

Wiki iliyopita, maaskofu hao walisema wanajua mshindi wa uchaguzi, tangazo lililolotafsiriwa na wengi kama onyo kwa mamlaka dhidi ya wizi wa kura.

Kabund alimtaja Tshisekedi kama mshindi wa uchaguzi huo, lakini hakusema alikuwa anajengea hoja yake kwa msingi gani. Kambi ya Shadary ilisema inatarajia kushinda huku kampeni ya Fayulu pia ikisema alikuwa katika nafasi imara ya kuibuka mshindi.

Kasoro zajitokeza

Wakati huohuo, ujumbe wa uangalizi wa uchaguzi huo ulisema Jumanne kuwa ulishuhudia kasoro 52 kubwa katika vituo 101 vya kuhesabu kura ulikotuma waangalizi, ikiwa ni pamoja na watu kuchezea matokeo.

Kuna vituo 179 vinavyoendelea kukusanya matokeo nchini Congo kote. Ripoti kutoka Shirika la SYMOCEL lenye makao yake nchini Congo imesema asilimia 16 a vituo vya vya kuhesabu kura lilivyoshuhudia vilitegemea matokeo kutoka kwenye mashine badala ya kura zilizohesabiwa kwa mkono kama inavyotakiwa kisheria.

Shirika hilo lilisema asilimia 92 ya vituo vya kuhesabia kura lilivyosimamia havikubandika fomu za matokeo nje kama inavyotakiwa kisheria.

Advertisement