MJADALA WA BAJETI ZA WIZARA: Wapinzani wahoji uhamishaji fedha

Dodoma. Wabunge wa upinzani jana walihoji mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na utaratibu wa kuidhinisha uhamishaji wa fedha, na sababu za kutokabidhiwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kutotengwa kwa fedha za kumalizia mchakato wa Katiba mpya.

Mambo mengine yaliyohojiwa na wabunge hao ni bendera za Chadema kuondolewa katika maeneo ambayo anapita Rais John Magufuli, matendo yanayofanywa na mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya dhidi ya mwenyekiti wa mbunge wa Hai, Freeman Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho.

John Mnyika, ambaye ni mbunge wa Kibamba, ndiye aliyeongoza maswali hayo akitaka kujua matumizi ya Sh976.96 bilioni, huku mengine yakihojiwa wakati wakiomba mwongozo katika mjadala wa bajeti ya Tamisemi na ya Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) mwaka 2019/2020.

Hoja hizo zilitolewa ufafanuzi na mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, huku mara kadhaa mawaziri na wabunge wa CCM wakisimama kuomba kutoa taarifa na utaratibu kwa lengo la kuwapinga.

Wabunge wengine waliohoji ni John Mnyika (Kibamba), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Lucy Kihwelu (viti maalum).

Matumizi Sh976.96bilioni

Chenge alilazimika kuomba kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard) ili kufuatilia na kutoa majibu ya hoja ya Mnyika aliyeitaka Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kueleza matumizi ya Sh976.96bilioni.

“Nitaomba kupata ufafanuzi kutoka ofisi ya Rais, ripoti iliyopita ya CAG iliibua madudu mengi katika sekta na wizara mbalimbali na kati ya mambo yaliyoibuliwa ni pamoja na Sh1.5trilioni na kupanda hadi 2.4trilioni,” alisema Mnyika.

Alisema Serikali iliwahi kufafanua kuwa Sh976.96 bilioni zilihamishwa kutoka mafungu tofauti na kupelekwa fungu la 20 ambalo ni Ofisi ya Rais Ikulu.

“Kama mbunge, naamini Bunge halikupitisha uamuzi wa kuhamisha fedha hizo kupeleka Ikulu.”

Lakini Chenge aliingilia kati. “Hebu nisaidie Sheria ya Bajeti kuhusu kuhamisha fedha inasemaje, ni Bunge linafanya au mamlaka husika?” alisema Chenge

Akifafanua suala hilo, Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji naye alisema: “(Mnyika) Athibitishe kwamba CAG anabanwa kukagua fungu 20 la ofisi ya Rais kwa sababu kinachofahamika kila fungu lina resident auditor kutoka ofisi ya CAG likiwemo fungu 20.

“Hakuna fungu hata moja ambalo CAG anazuiwa kukagua na fungu hili lilikaguliwa. Hoja zake anawadanganya Watanzania, anamchafua Rais bila sababu za msingi.”

Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga alisema kwamba kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) inayoongozwa na upinzani imeeleza hakukuwa na tofauti ya matumizi ya Sh1.5 trilioni na kumuomba Chenge kulimaliza suala hilo.

Kutokana na Mnyika kuendelea kushikilia hoja yake, Chenge alisema mbunge huyo ni kama anawapotezea muda na kuagiza kupata taarifa za kumbukumbu za Bunge ili kufuatilia vyema hoja yake na kwamba uamuzi utatolewa leo saa 7:00 mchana.

Mnyika pia aliibuka na hoja ya CAG, akisema wabunge hawajapewa ripoti za ukaguzi za mwaka 2017/18 na kutaka kikao cha Bunge kusitishwa suala hilo lijadiliwe.

“Jambo hili linaminya haki yetu,” alisema Mnyika.

Chenge alisema kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu taarifa za CAG zina utaratibu wake wa kuwasilishwa, akisisitiza kuwa Serikali iliziwasilisha na kuzionyesha.

“Mwongozo wangu kwa suala hilo kwa mujibu wa kanuni ya 51 namuuliza Mnyika anionyeshe ni kifungu gani cha sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kinachoonyesha hizi zikiwasilishwa hapa lazima zigawiwe kwa wabunge?” alihoji.

“Uamuzi wangu ni kwamba Serikali itawasilisha kwa wabunge kupitia taratibu zetu kwa wakati muafaka.”

Kura ya Maoni yaibuka

WMnyika pia alihoji sababu za Serikali kutotenga fedha kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa kura ya maoni kupitisha Katiba Inayopendekezwa.

“Ofisi ya Rais imkumbushe (Rais) kwamba hatua iliyofuata ni kura ya maoni kupitisha Katiba mpya, ni muhimu katika majumuisho ofisi ya rais ikasema kwanini katika Bunge hili haijatengwa fedha kwa ajili ya kura ya maoni na kupitisha katiba,” alisema Mnyika.