Wapinzani waibua bungeni matukio ya utekaji, mauaji

Dodoma. Hoja ya mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kuitaka Serikali kueleza kwa kina na uwazi kuhusu uchunguzi wa matukio ya watu kutekwa, kupotea na kuuawa nchini, juzi ilitikisa Bunge huku Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akitoa majibu yaliyopingwa na wabunge wa upinzani.

Wakati wapinzani wakipinga majibu ya Lugola, wenzao wa CCM waliungana na waziri huyo aliyesema kuwa uchunguzi wa matukio hayo unaendelea na wahusika wakikamatwa watafikishwa mahakamani.

Mvutano huo ulitokea juzi jioni wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani mwaka 2019/2020 baada ya Msigwa kushika shilingi akiitaka Serikali kutoa majibu ya kina kuhusu matukio hayo.

Tukio la mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kupigwa risasi; kutoweka kwa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Azory Gwanda; kuuawa kwa aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Geita, Alphonce Mawazo; kutekwa kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ na mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye kutishiwa bastola ni matukio yaliyotumika kama mfano wakati wabunge wakijadili hoja hiyo ya Msigwa.

Katika mjadala huo, Nape alikumbushia tukio la kutishiwa bastola mwaka 2017 akisisitiza kuwa licha ya kumjua mhusika ambaye alifanya kitendo hicho mbele ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa na Wilaya, hadi sasa bado hajakamatwa.

Ilivyokuwa

“Katika tukio la kutekwa kwa ‘Mo’ Rais aliwahi kulieleza Jeshi la Polisi kuwa Watanzania si wajinga, kuna tukio la Lissu mnasema dereva wake kutopatikana ndio sababu ya kushindwa kufanya upelelezi, huyu Nape wapi amehojiwa tangu alipotishiwa bastola hadharani,” alihoji Mchungaji Msigwa.

“Azory ripoti ipo wapi, polisi tunawapenda sana na tunawahitaji lakini tunataka Jeshi hili tuwe na imani nalo, ni lini wanatoa maelezo ya kina na wazi kwa matukio makubwa?”

Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alipomtaka Lugola kutoa majibu ya Msigwa, waziri huyo alisema polisi inaendelea na uchunguzi wa matukio hayo na ukikamilika taarifa itawekwa wazi huku akisema kuwa Nape alitakiwa kuripoti polisi baada ya kutishiwa bastola.

“Sijaridhika na majibu ya Kangi naomba nitoe hoja wabunge tujadili,” alisema Mchungaji Msigwa.

Akichangia hoja hiyo mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko alisema wakati Serikali ikishindwa kutoa majibu kuhusu Mawazo na Lissu, polisi iliweza kuwakamata wanaodaiwa kumpiga risasi aliyekuwa kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow kisha akahoji, “mbona wengine hawakamatwi?”

Mbunge wa Siha (CCM), Dk Godwin Mollel alipingana na hoja ya Msigwa akisema tukio la Lissu uchunguzi hauwezi kufanyika kwa kuwa dereva aliyekuwa naye kwenye gari hayupo.

Dk Mollel aliungwa mkono na mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga aliyesema uchunguzi wa matukio hayo hauwezi kuletwa bungeni, hupelekwa mahakamani na watuhumiwa kusikilizwa na hukumu kutolewa.

Kwa upande wake, mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alisema, “jinsi tunavyojadili hili jambo tunazidi kuifedhehesha Serikali na polisi, waziri alivyozungumza kama wana tetesi na mhusika kwa nini asikamatwe.”

“Dereva (wa Lissu) alikuwa Kenya, lakini siku ya tukio (mbunge huyo alipopigwa risasi) nilikuwa na RCO ndio aliniomba mimi nimtafute dereva akatoe gari na liliondolewa, mlikuwa mnamtafuta dereva kwa nini asipatikane.”

Alisema uchunguzi kuhusu shambulizi la Lissu ungeweza kufanyika kwa risasi zilizotumika kuchuguzwa zimenunuliwa wapi, ni za silaha gani na zinatumiwa na nani.

Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche alisema, “tunataka majibu ya akina Azory yuko wapi, nani waliomuua Mawazo. Nyinyi ndio wenye vyombo vya uchunguzi.”

Wakati Heche akieleza hayo, mbunge wa Serengeti (CCM), Marwa Ryoba alitaka Heche na wabunge wa Chadema kukamatwa na kuhojiwa kuhusu tukio la Lissu kupigwa risasi kwa madai kuwa wamemficha dereva wa mbunge huyo.

Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh aliwakumbusha wenzake kuacha kumtolea mfano Lissu pekee kwa kuwa matukio ya utekaji, watu kupotea na kuuawa ni mengi.

“Lissu ni mmoja tu, tunachodai Serikali kutumia fursa hii kulisafisha jeshi (la polisi). Anachotaka Msigwa tusifanye siasa, hii ni kwa ajili ya nchi yetu, mfano polisi walisema kesi ya Akwilina (Akwilini-aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji-NIT) imefungwa ingawa kuna wengine walishtakiwa wakati kesi imefungwa,” alisema.

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Sophia Mwakagenda alisema hakuna ajuaye nani atafuata kutekwa na wanaosema Chadema inahusika na tukio la Lissu ndio waliokataa wazo la chama hicho tukio hilo kuwapo kwa uchunguzi na wachunguzi wa kimataifa.

Mbunge wa Mwanakwerekwe (CUF), Ali Salim Khamis alitolea mfano kutekwa kwa Ally Juma Selemani na kutupwa porini kisha kufariki siku tatu baadaye akiwa hospitali, pamoja na mpigakura wake aliyechukuliwa dukani miaka miwili iliyopita na hadi sasa hajulikani alipo.

Kwa upande wake, Nape alisema mtu aliyemtishia bastola amekuwa akitajwa kwa jina lake na kazi anayoifanya, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Nape alikumbana na kadhia hiyo Machi 23, 2017 ikiwa ni saa chache tangu Rais John Magufuli alipotangaza kumuondoa kwenye Baraza la Mawaziri alikokuwa akihudumu kama Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Baada ya kuondolewa asubuhi, siku hiyohiyo mchana Nape alipanga kufanya mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam, ambako alikuta zuio la vyombo vya dola na alipolazimisha alijikuta akitolewa bastola mbele ya wanahabari wa ndani na nje akitakiwa kurudi ndani ya gari lake.

“Ninaamini (mtu huyo) hakutumwa na Serikali, alifanya kwa ujinga wake wa kutotumia busara kutekeleza kazi aliyotumwa. Serikali ni vizuri ikajitenga na matukio haya, busara ndogo ya kumaliza mambo haya ili wanaotumwa kutekeleza majukumu wakatumia busara,” alisema Nape.