VIDEO: Wapinzani waipeleka Serikali ya Tanzania mahakamani

Muktasari:

  • Vyama vinane vya upinzani vimepinga mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa na tayari Serikali imepewa siku 45 kujibu madai hayo.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imepewa siku 45 na Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) kujibu madai ya vyama vinane vya upinzani vinavyopinga Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, baada ya vyama hivyo kufungua kesi Februari 12, 2019.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 15, 2019 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kesi hiyo Na.3 ya 219 imefunguliwa na yeye mwenyewe na wenzake akiwemo Naibu Katibu mkuu wa chama hicho (Zanzibar), Salum Mwalimu, Maalim Seif Sharif Hammad na Zitto Kabwe wa ACT Wazalendo.

Amesema sheria hiyo inakiuka vifungu vya 6,7 na 8 vya Mkataba wa Afrika mashariki ikiwa ni pamoja na kuminya demokrasia nchini.

"Kwanza tunapinga sheria yenyewe na pili tunaiomba Mahakama ya Afrika Mashariki iizuie sheria hiyo isitumike hadi kesi ya msingi isikilizwe," amesema Mbowe.

Amesema hatua ya kufungua kesi imekuja baada ya hatua nyingine ikiwa ni pamoja wadau kutoa maoni yao.

"Sheria hiyo ime-criminalize (imeharamisha) demokrasia nchini. Wakati nikiwa gerezani wenzangu walikubaliana mambo kadhaa. Kwanza kuweka msukumo mkubwa kwa sheria hiyo," amesema.

"Bahati mbaya sheria ilipitishwa, licha ya maoni ya wadau, sheria ilipitishwa. Ni kiburi kilichopitishwa. Ilitusikitisha sana maana yake washindani wetu wanakuwa waamuzi," amesema.

Mbowe amesema wamefungua kesi hiyo EACJ kabla ya mahakama za ndani kwa kuwa kulikuwa na kikomo cha siku za kufungua shauri hilo, kisha watafungua kesi mahakama za ndani.

Hata hivyo, vyama sita ndivyo vilivyokuwepo kwenye kutia saini makubaliano ya kesi hiyo wakiwemo Chadema, ACT Wazalendo, Chaumma, CCK, NLD na UPDP.