Wapinzani walia na taulo za kike, mawigi

Wednesday June 26 2019
pic wapinzani

Kaimu Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde akiwasilisha maoni kambi hiyo kuhusu muswada wa sheria ya Fedha wa mwaka 2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema Serikali ya Tanzania imeshindwa kutambua vyanzo vipya vya mapato kwa kung’ang’ania kodi katika taulo za kike na kuongeza ushuru katika nywele bandia ‘mawigi.’

Katika bajeti ya Serikali mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni, Serikali ya Tanzania imerejesha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye taulo za kike kwa madai ya walengwa kutonufaika.

Pia, itaanza  kutoza ushuru wa asilimia 10 kwa nywele  bandia zinazotengenezwa nchini na asilimia 25 kwa zinazoingizwa kutoka nje.

Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde akiwasilisha maoni ya kambi hiyo leo Jumatano Juni 26, 2019 kuhusu muswada wa sheria ya fedha mwaka 2019 kwa niaba ya waziri kivuli wa Wizara ya Fedha, Halima Mdee, amesema ikitokea wanawake wote wakaamua kunyoa nywele na kutovaa nywele bandia, Serikali haitapata mapato.

“Jambo hili si sawa kwa sababu ni mapato yanayotarajiwa kupatikana kutoka kwa mama zetu kwa sababu tu wao ni wanawake na watumiaji wakubwa wa nywele bandia.”

“Maoni yetu ni kwamba kifungu hiki kifutwe na Serikali itafute vyanzo vingine vya mapato vinavyotokana na rasilimali za Taifa hili,” amesema Silinde.

Advertisement

Kuhusu taulo za kike, Silinde amesema haiungi mkono Serikali kutumia hedhi kama chanzo cha mapato ya Serikali.

“Tunapendekeza kifungu hiki kifutwe na Serikali itimize wajibu wake wa kuhakikisha wanufaika wa taulo za kike wananufaika wenyewe badala ya wafanyabiashara, wajibu huo ni wa Serikali na kamwe haiwezekani kushindwa kutekelezwa kwa wajibu wa Serikali ikiwa ni kwa gharama za hedhi ya wanawake wa Tanzania,” amesema Silinde.

Advertisement