Wapinzani wamuunga mkono Nape

Dar es Salaam. Kauli aliyotoa Nape Nnauye kuwa “hakuna CCM imara kama hakuna upinzani imara” imepokelewa vizuri na wanasiasa wa upinzani na wasomi, ambao wamekitaka chama hicho tawala kuitafakari na kuifanyia kazi.

Wamesema ili chama hicho tawala kiweze kujipima kikamilifu kwa yale kinayoyafanya kwa wananchi, ni lazima kuwepo na kioo cha kujiangalia, ambacho walisema ni vyama vya upinzani.

Nape, mbunge wa Mtama aliyekulia ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM, alitoa kauli hiyo juzi alipoalikwa katika kipindi cha 360 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds TV.

Waziri huyo wa zamani alisema siasa hazitakiwi kuwa ugomvi bali kushindana kwa hoja.

“Hakuna CCM imara kama hakuna upinzani imara. Tunategemeana na namna ya kutegemeana ni kushindana kwa hoja,” alisema Nape katika kipindi hicho cha mazungumzo.

HABARI ZAIDI HAPA

“Kwenye siasa nadhani tusiende kwenye kugombana bali kubishana kwa hoja na inapotokea mnapishana iwe ni kwenye kuboresha si kuchukiana na mabishano hayo si mabaya wala uadui na isichukuliwe kwamba mtu anayejadili kwa misimamo hiyo asionekane anapinga.”

Ametoa kauli hiyo wakati vyama vya upinzani vikilalamikia kuminywa, huku vikituhumu kuwepo kwa mpango wa kuviua kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2010.

Vyama hivyo vinalalamikia viongozi wake kupishana mahakamani na polisi kutokana na tuhuma mbalimbali, kuzuia kufanya siasa na vilisusia uchaguzi mdogo mkatika maeneo tofauti kwa madai kuwa wagombea na mawakala walikuwa wanakamatwa.

“Kauli ya Nape ina mashiko sasa na kabla na itaendelea kuwa hivyo,” alisema kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe.

“Kama chama tawala kikiwa hakina upinzani itakuwa ni nchi ya hovyo kwa sababu hakitakuwa na maelewano na kitakuwa na ugomvi kwa kuwa upinzani uliokuwa nje utahamia ndani,.”

Mtazamo wa Zitto unafanana na wa mwenyekiti wa Baraza la Katiba Zanzibar, Profesa Abdul Sherrif aliyesema CCM inatakiwa kutafakari na kuifanyia kazi kauli hiyo.

“Mchango unaotolewa na wabunge wa upinzani ni mkubwa na unaifanya CCM na Serikali yake iwajibike kwa wananchi,” alisema Profesa Sherrif aliyewahi kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Lakini Dk Richard Mbunda wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora wa UDSM, alienda mbali zaidi aliposema hata upinzani unahitaji kuwa imara zaidi.

“Kwa sababu upinzani imara hausababishi kuwa na CCM imara tu bali ndiyo tunapata Bunge imara kwa idadi ya wabunge wenye mawazo mbadala,” alisema Dk Mbunda.

“Ndiyo tunapata Serikali imara na inayowajibika ipasavyo kwa wananchi,” alisema Dk Mbunda.

Kuhusu mchango wa upinzani imara ulivyochangia uwajibikaji wa Serikali, mhadhiri huyo alisema kashfa nyingi zilizoibuliwa nchini, zimetokana na kazi ya upinzani, akitoa mfano wa sakata la Escrow, EPA na Richmond.

Alisema kwa miaka mingi, Serikali chini ya CCM imekuwa ikiwajibisha viongozi wake kama mawaziri kutokana na kashfa zinazoibuliwa na upinzani.

Mmoja wa viongozi wa juu wa CCM ambaye hakupenda kutajwa jina kwa madai kuwa “viongozi wakubwa hawatakiwi wajibizane, alisema kauli ya Nape ni mtazamo wake.

“Kila mmoja ana mtazamo wake kwenye medani za siasa. Kwake yeye kaona hivyo inawezekana mwingine asione, akatae kabisa au aunge mkono,” alisema kiongozi huyo.

Lakini mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe hakuunga mkono kauli hiyo, akisema haina mashiko.

“Inawapasa wafikirie wenyewe badala ya kuwaambia upinzani,” alisema mwanasheria huyo.

“Sisi tunalijua hilo siku nyingi na ndiyo maana ni watulivu. Wao ndiyo wanapaswa watafakari na wajikumbushe mara kwa mara jinsi walivyokuwa wakifanya mambo kwa mazoea walipokuwa hawasimamiwi.

“Baada ya kelele za upinzani ndiyo wanajaribu kusutana kila siku.”

Rungwe alisema mara zote CCM wamekuwa wakiwahadaa wananchi kuwa wameshinda ilihali wanajua hawajashinda. Siku wakilipuka hali itakuwa mbaya.

“Tunapambana kuhakikisha wanaelewa maana ya siasa safi na bora, ndiyo maana tunapinga wakurugenzi kusimamia uchaguzi. Haiwezekani refa wao, mpira wao, uwanja wao halafu wafungwe. Pia tunataka hata spika awe huru asitoke chama chochote ili kuwe na usawa kule bungeni,” alisema Rungwe.

Naye naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema mwanasiasa yoyote makini lazima atatambua jambo hilo.

“Uimara wako wewe utaupima kutokana na mwenzako. Haiwezi kuwapo CCM imara kama hakuna upinzani imara, hata sisi siku tukishika dola hatutavunja upinzani, tutaacha ushamiri kwa mujibu wa sheria taratibu na maadili tulichojiwekea,” alisema Mwalimu.

Alihoji CCM inajipimaje wakati imewafunga wapinzani mikono na miguu.