Wapinzani wana siku 20 kupinga sheria ya vyama vya siasa EACJ

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema wanaendelea na vikao na vyama 10 pamoja na wadau wengine ili kupeleka kesi hiyo ndani ya wakati.

Dar es Salaam. Vyama vya upinzani na wadau wanaopinga marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wanazo siku 20 kupeleka kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), tangu marekebisho hayo yaliposainiwa na Rais John Magufuli Februari 13 na kuchapishwa ndani ya Gazeti la Serikali Februari 22.

Marekebisho hayo yalizua mjadala mzito yalipopelekwa kama muswada bungeni mjini Dodoma mwishoni mwa 2018.

Msemaji wa EACJ, Anna Nabata alisema utaratibu wa mahakama hiyo ni kupokea kesi moja kwa moja kutoka kwa walalamikaji na kama ni kupinga sheria inatakiwa iwe ndani ya miezi miwili tangu mlalamikaji alipojua.

“Mtu anaweza kuleta kesi moja kwa moja bila kupitia mahakama za ndani. Kama ni kupinga sheria inatakiwa ije ndani ya miezi miwili tangu mlalamikaji alipojua,” alisema Nabata.

Hii ina maana kuwa miezi miwili kuanzia Februari 13 itamalizika Aprili 14.

Tayari Chadema wameshaonyesha nia ya kupeleka kesi mahakamani kupinga marekebisho hayo wakihusisha vyama na wadau wengine wa demokrasia.

Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema wanaendelea na vikao na vyama 10 pamoja na wadau wengine ili kupeleka kesi hiyo ndani ya wakati.

“Kesi yetu itaanzia mahakama za ndani na hatuko peke yetu. Kwa Mahakama ya Afrika Mashariki hadi wiki ijayo tutakuwa na mwelekeo wa hiyo kesi,” alisema Mrema.

Hata hivyo, wakili maarufu nchini, Jebra Kambole alisema kesi katika mahakama hiyo huchukua hadi miaka miwili kusikilizwa na kutolewa uamuzi.

“Ni muhimu kwenda Mahakama ya Afrika Mashariki kwa sababu kuna mkataba ambao Tanzania imeridhia na moja ya vipengele ni kuimarisha demokrasia. Kwa hiyo unaweza kupinga sheria hiyo kwa kuwa inapinga mkataba huo,” alisema Kambole.

“Kwa sasa mahakama hii ina mrundikano wa kesi na majaji wake hukaa kwa vipindi vitatu kwa mwaka, kwa hiyo kesi inaweza kuchukua hata miaka miwili. Lakini bado kuna matumaini kwa sababu mapambano ya demokrasia yatasaidia vizazi vijavyo.”

Kuhusu mahakama za ndani, Kambole alisema kesi kama hiyo huchukua kipindi cha mwaka mmoja kusikilizwa hadi kutolewa hukumu.

Sababu ya kupinga

Akizungumzia sababu ya kupinga, Kambole alisema sheria hiyo ina dalili za kwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Uhalali wa sheria ni kuendana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Mimi naamini sheria hii inapingana na Katiba na ni kikwazo cha ufanyaji wa siasa, kwa mfano inapozungumzia madaraka ya msajili, watu wanapoungana kufanya siasa na utoaji wa elimu ya uraia,” alisema.

“Sheria hii inavunja haki ya kushiriki siasa inayotolewa na Katiba ibara ya 21 na ibara ya 20 inayotoa haki ya kukusanyika na kujiunga na vyama. Kwenye utoaji elimu ya uraia kuna wadau wengi wanahusika, lakini wamebanwa.”

Alisema wapinzani wa sheria hiyo wanatakiwa kutumia ibara ya 26(2) wanapofungua kesi yao. Kifungu hicho kinasema; “Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za nchi.”

Maoni ya Kambole yanaungwa mkono na Wakili Awadhi Said wa Zanzibar aliyeongeza kifungu cha 30(5) kinachosema kama Mahakama Kuu ikiridhika kwamba sheria husika inakwenda kinyume cha Katiba, inaweza kuchukua hatua.

Mbali na kupinga sheria hiyo, Wakili Onesmo Kyauke alisema hata Msajili wa Vyama vya Siasa anaweza kushtakiwa kwa kuangalia mapitio ya kisheria (judicial reviews).

“Hata kama sheria imesema msajili hawezi kushtakiwa, inawezekana kumshtaki kwa kupitia judicial reviews na ndiyo hivyo unaweza kuishtaki Tume ya Uchaguzi inapomtangaza mshindi wa kiti cha urais hata (kama) sheria hairuhusu,” alisema.

“Unachoshtaki pale sio usahihi, bali ni uhalali wa uamuzi. Hata Rais anaweza kushtakiwa kwa kuangalia uhalali wa maamuzi anayofanya. Kuna watu wameshashtaki kuhusu hati za umiliki wa ardhi na wameshinda.”

Kuhusu marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa, Kyauke aliungana na wenzake akisema kuna vipengele vinavyokinzana na Katiba.

“Kwa mfano Katiba inatoa haki ya uhuru wa kukusanyika, vyama vimeamua kuungana vyenyewe, lakini sheria inatoa masharti kinyume,” alisema wakili huyo.