Wasiosafisha mahindi ya dona hatarini kuugua saratani ya ini

Friday March 15 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imesema ulaji wa vyakula vilivyochafuliwa na kiasi kikubwa cha sumukuvu husababisha madhara ya kiafya ya muda mfupi na muda mrefu.

Madhara ambayo mtu anaweza kuyagundua baada ya muda mrefu kupita ni ya kuugua saratani ya ini na madhara ya muda mfupi ni mlaji kuugua ugonjwa wa kuhara.

Sumu hiyo hupatikana kwenye mazao ya nafaka hasa mahindi na karanga, na kwamba walaji wa ugali wa dona wapo hatarini zaidi ikiwa hatua za uandaaji wa chakula hicho hautazingatiwa.

Hayo yalizungumzwa jana na msemaji wa TFDA, Gaudensia Simwaza alipoulizwa kuhusu hatua zinazochukuliwa kudhibiti waandaaji wa unga wa dona nchini na madhara yanayoweza kumpata mtu endapo atakula chakula hasa ugali wa dona ambayo imechafuliwa na sumu kuvu. Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga juzi wakati akizindua mradi wa kudhibiti sumukuvu (Tanzania Initiative Preventing Aflatoxin Contamination - Tanpac), alitoa tahadhari kwa Watanzania wanaosaga dona bila kuosha mahindi.

“Ijulikane kuwa dona ina lishe na ni sahihi kuliwa, shida ni maandalizi ya unga wa dona tunachosema kwanza ni lazima anayeandaa aoshe kwa umakini na usahihi kwani wengi huhifadhi mahindi na dawa,” alisema Simwaza.

Alisema TFDA imekuwa ikitoa maelekezo kwa wamiliki wa viwanda vyenye mashine na watu mbalimbali, “tumekuwa tukiwapa mafunzo na hata wanaofungasha wapo wazalishaji lakini hawana mashine, hawa tunawapa mafunzo namna ya kuandaa dona ili uwe unga utakaotumika na watu bila kuleta madhara.”

Alisema TFDA inatambua tatizo, lakini pamoja na mambo ya utafiti mbalimbali ni moja ya eneo ambalo wanalipa kipaumbele. “Tumekuwa tukielimisha wananchi Dodoma na Manyara mwaka 2016 baadhi ya watu kama 80 walipata madhara mbalimbali kutokana na sumukuvu, lakini tulihakikisha wanapatiwa elimu katika vijiji husika, hivi sasa maeneo yale wana elimu kubwa hata jamii tumekuwa tukiielimisha kuhusu sumu kuvu,” alisema Simwaza.

Advertisement