Wasomi, wananchi waukosoa

Friday November 14 2014Dk Benson Bana

Dk Benson Bana 

By Kelvin Matandiko na Goodluck Eliona, Mwananchi

Dar es Salaam. Baadhi ya wasomi nchini, wameukosoa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Twaweza kwamba hakuakisi uhalisia, huku wengine wakihoji mfumo wa utafiti wakisema hauwezi kuleta majawabu yanayoakisi hali halisi.

Kwa mujibu wa Twaweza, utafiti huo umefanywa kimakundi ukizingatia uwakilishi wa kitaifa kwa njia ya simu ya mkononi. Kanuni ya msingi ni kuwa na makundi mawili ya wahojiwa kutoka mijini na vijijini.

“Sampuli za kaya 2,000 zilitengenezwa kupitia hatua tatu, kwa kutumia uchunguzi nasibu kila hatua; kwanza, maeneo ya kuhesabia 200 yalichaguliwa, kisha kaya 10 zilichaguliwa kinasibu kutoka kwenye orodha ya kaya zote katika eneo la kuhesabia, kisha mtu mzima mmoja alichaguliwa,” yanasomeka maelezo ya Twaweza nakuongeza:

“Kila kaya ilipatiwa simu ya mkononi na chaja inayotumia nishati ya jua. Wakala wa kituo cha kupigia simu huwasiliana na kila kaya kila mwezi na kuwauliza maswali yanayohusu mada na masuala mbalimbali”.

Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (Ruco), alisema utafiti umeshindwa kutaja sifa zilizowafanya baadhi ya wanasiasa kutajwa kwamba wanafaa kushika madaraka ya urais, hivyo kuegemea kwa watu zaidi na kusahau mfumo na sera za nchi.

Profesa Mpangala alisema wagombea wote waliojitokeza kwa tiketi ya CCM na kutajwa katika utafiti huo hakuna anayefaa kuwa rais kwa kuwa hawawezi kupambana na ufisadi na rushwa iliyokithiri nchini.

Advertisement

“Mchakato wa Katiba Mpya umepitishwa kwa masilahi ya chama na watu binafsi siyo maoni ya wananchi. Hilo ni tatizo langu ndiyo maana nasema hizi ni propaganda,” alisema Profesa Mpangala.

Akizungumzia hoja kwamba hata vyama vyote vya upinzani vikiungana haviwezi kuiangusha CCM, alisema ripoti hiyo imepotosha kwa kuwa kuna mifano mingi ya vyama tawala vilivyong’olewa madarakani.

“Kwa nini wanasema hawawezi kuishinda CCM hata wakiungana? Kenya vyama viliungana vikaing’oa Kanu, Zambia nako vyama vilifanya hivyohivyo, suala hapa vyama vya upinzani viwe na mikakati mizuri na vitoe taarifa kwa wananchi,” alisema.

Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikosoa njia ya ukusanyanyi maoni iliyotumiwa na Twaweza kwa madai kuwa ina kasoro nyingi, hasa pale mtu anapopewa simu ili aweze kuhojiwa.

Hata hivyo, kauli yake hiyo inapingana na msimamo wake alioutoa juzi wakati wa uzinduzi wake, aliposema utafiti huo ni wa kitaalamu hivyo kuupinga lazima ufanyike utafiti mwingine na siyo vinginevyo.

Profesa Goerge Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema matokeo ya utafiti huo hayawezi kuhalalishwa moja kwa moja kuwa ni halisi ya uchaguzi ujao, kwani kutakuwa na mabadiliko makubwa ndani ya CCM na harakati za Ukawa.

Alisema ushindani ndani ya CCM bado ni mkubwa ikilinganishwa na makundi yanayojitangaza sasa.

“Mambo yanaweza kubadilika, CCM ina hazina kubwa na ninaamini hali inaweza kubadilika kwani kuna vigogo ndani ya CCM ambao wanaweza kujitokeza watu wakashaangaa na wakaonekana kuwa na mvuto kuliko hawa wa sasa,” alisema.

Kuhusu nafasi ya Ukawa, Profesa Shumbusho alisema kundi hilo bado lina nafasi nzuri na kwamba matokeo hayo hayawezi kulikatisha tamaa katika harakati zake.

“Jambo linaloweza kuwanusuru Ukawa ni umoja wao lakini sidhani kama wanaweza kuvumiliana mpaka uchaguzi ujao, wakiendelea hivyo kwa sasa wanaweza kuongeza asilimia za kundi la waliosimama katikati,” alisema Profesa Shumbusho.

Akichambua matokeo ya jumla katika ushindani wa nafasi ya urais kwa mgombea mmoja mmoja, alisema endapo utafiti huu hautapingwa na mwingine, basi nafasi ya matokeo hayo inaweza kutarajiwa.

“Lakini tunahitaji tafiti nyingine zijitokeze zaidi kabla ya uchaguzi ili kuona kama utakuwa tofauti na matokeo au utakuwa sawa na huu, vinginevyo Watanzania wanaweza kubadilika wakati wowote ndani ya mwaka mmoja kabla ya uchaguzi,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Emmanuel Mallya alisema ni mapema mno kupata uhakika nani anaweza kuingia Ikulu 2015... “Bado muda upo, mabadiliko yanaweza kutokea lakini hayawezi kuwa na tofauti kubwa.”

Wananchi wengine

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), Mussa Mdede alisema utafiti huo ni mwendelezo wa vita na mvutano mkubwa ndani ya ushindani wa vigogo wa CCM... “Ikitokea kundi lililoongoza katika utafiti huo likashindwa ndani ya uchaguzi wa NEC, itasababisha mpasuko mkubwa. Pia hata Ikulu ina kundi lake, hivyo sidhani kama utafiti huo unaweza kuwa sawa na matokeo hayo.”

Kuhusu Ukawa, Mdede alisema utafiti huo umetoa mwelekeo kwamba kundi hilo lina nafasi kubwa ya kuungwa mkono na watu ambao hawajafanya uamuzi.

“Ukichukua asilimia 28 waliyoipata kabla ya kuungana, wanayo nafasi ya kuteka kundi asilimia 6 wasiojua lolote na asilimia 16 ya wanaotaka mgombea na siyo chama kwani wote hao wameonekana kuchoshwa na mfumo wa utawala uliopo.

“Kwa hivyo ninaamini watakuwa fursa endapo hali itaendelelea hivi. CCM umaarufu wao hauwezi kuwa juu ya muungano wa Ukawa kwa sasa kutokana na changamoto za udhaifu wa Serikali.”

Mfanyabiashara wa Kijitonyama, Dar es Salaam, Leonard Mkenda alisema hakubaliani na matokeo ya ripoti hiyo kwa kuwa yameacha maswali mengi kuliko majibu, huku akihoji kwa nini watafiti waliamua kuuliza wananchi 1,445 pekee wakati kulikuwapo na uwezekano wa kuwahoji wengi zaidi.

Mkenda alihoji kwa nini wananchi waliopigiwa simu hawakutajwa majina yao ili kuondoa hofu kuwa waliohojiwa wanatoka sehemu moja, pia ni wanachama wa chama kimoja.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum alisema ushindani wa makundi ndani ya CCM, hautabiriki hivyo matokeo hayo hayawezi kuwa majibu sahihi ya uchaguzi mkuu ujao.

Kuhusu nafasi ya Ukawa, Sheikh Salum alisema nafasi yao ya ushawishi haitaweza kuongezeka na badala yake inaweza kushuka kutokana na utamaduni Watanzania kushawishiwa na aina ya chama na siyo muungano wala mgombea.

Advertisement