Wasomi wamjibu Lugola, wataka uchunguzi huru shambulio la Lissu

Muktasari:

Siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kulishangaa Jeshi la Polisi kushindwa kumkamata mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu wakati linawakamata vijana kwa uzururaji, wasomi nchini Tanzania wamekata kuwe na chombo huru cha kuchunguza tukio la mbunge huyo kupigwa risasi


Dar es Salaam. Baadhi ya wanasheria na wachambuzi wa masuala ya siasa wamesema kuna umuhimu wa kuwa na chombo huru kuchunguza shambulio la mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.

Maoni hayo ya wasomi yamekuja siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kulishangaa Jeshi la Polisi kushindwa kumkamata mbunge huyo wakati linawakamata vijana kwa uzururaji.

Lissu alishambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 jijini Dodoma, siku moja baadaye alisafirishwa kwenda Nairobi,  Kenya kabla ya kuhamishiwa nchini Ubelgiji anakoendelea na matibabu licha ya kuruhusiwa kutoka hospitali Desemba 31, 2018.

Lissu kwa sasa yupo katika ziara nchini Marekani akieleza kuhusu shambulio lake hilo, kuzungumzia masuala ya siasa na utawala nchini.

Wakizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Februari 14, 2019 mwanasheria Harold Sungusia amesema hakutakuwa na mshindi hadi kitakapopatikana chombo huru kuchunguza na kutoa taarifa.

“Hauwezi kuwa jaji kwenye kesi yako mwenyewe katika ile ‘principle of natural justice’ (kanuni ya haki za asili). Kwa kuwa huyo mmoja anaituhumu Serikali na Serikali inamtuhumu mhusika, hapo inatakiwa kipatikane chombo huru,” amesema Sungusia.

“Kama mtu alipigwa risasi ijulikane na kama mtu anazungumza maneno ambayo ni kero kwa Serikali ijulikane. Kwa sababu kila mtu analalamika.”

Ameongeza, “Serikali haina moral authority (mamlaka) ya kuunda tume yake kwa sababu inatuhumiwa. Inaweza kuomba Jumuiya ya Madola kwa mfano au SADC (Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika) au ya Umoja wa Afrika kupitia mkataba wa Haki za Binadamu wa Afrika ili itoe ripoti.”

Hoja hiyo imeungwa mkono na mwanasheria mwingine,  Kainerugaba Msemakweli, “Lissu ni mgonjwa aliyetelekezwa tangu siku ya kwanza. Anajieleza jinsi alivyoshambuliwa na hapewi fedha za matibabu zaidi ya mshahara wake. Mpaka leo hakuna hata mtu mmoja aliyekamatwa,” amesema Msemakweli.

“Kuna suala la watu wasiojulikana, watu wametekwa, watu wamepotea ukiuliza wanasema ni watu wasiojulikana. Kama watu wasiojulikana wamewashinda basi walete kikosi kutoka nje ya nchi kichunguze.”

Mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda amesema, “Hapa tunamzungumzia mbunge, tunazungumzia kiongozi wa upinzani, ni Mnadhimu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni na amechaguliwa na wananchi. Halafu mtu huyo anashambuliwa kiasi cha kunusurika kufa, haya ni mambo makubwa.”

“Alishasema kuna watu wanamfuatilia mbona Polisi hawakuchukua hatua? Amesema pia kuwa ameshambuliwa eneo ambalo lina ulinzi mpaka leo hajakamatwa hata mtu mmoja? Inabidi Jeshi la Polisi litumie busara ya hali ya juu.”

Amesema kwenye mkataba wa kijamii, Jeshi la Polisi linapaswa kuhakikisha ulinzi wa raia wote hivyo Lissu yuko sahihi kudai kulindwa.

“Lissu yuko sahihi kwa sababu ana haki ya kulindwa. Kwenye mkataba wa kijamii kila mtu ana haki ya kulindwa, Serikali ionyeshe kufuatilia tukio hilo.”