Wataalamu wa maabara wajivua lawama vipimo UTI, zigo kwa madaktari

Muktasari:

  • Juzi, wataalamu kutoka Chama cha Wataalamu wa Maabara za Afya ya Binadamu (MeLSATT), walisema kuwa kipimo cha UTI hutoka kati ya saa 48 hadi 72.

Dar es Salaam. Wataalamu wa maabara wamejivua lawama kuhusu matokeo ya kipimo cha maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) kutoka ndani ya muda mfupi, wakisema kazi yao ni kupima tu.

Wametoa kauli hiyo baada ya Mwananchi kumkariri mganga mkuu wa Serikali akisema kuwa vipimo vya ugonjwa huo vinatakiwa vitoke kati ya saa 48 na 72, tofauti na hali ilivyo mitaani ambako matokeo ya vipimo hutoka muda mfupi baada ya kuchukuliwa.

Juzi, wataalamu kutoka Chama cha Wataalamu wa Maabara za Afya ya Binadamu (MeLSATT), walisema kuwa kipimo cha UTI hutoka kati ya saa 48 hadi 72.

Roman Stephen, mwenyekiti wa dawati la habari wa MeLSATT, alisema siyo jukumu la wataalamu wa maabara kusoma matokeo ya vipimo, bali ni daktari.

“Daktari ndiye mtu atakayetoa tafsiri ya majibu ya vipimo kwa mgonjwa kulingana na mpangilio wa matibabu alioamua kuufuata kwa kuzingatia utaalamu wake,” alisema Stephen.

Alisema chanzo cha malalamiko yaliyopo ni ishara kuwa kuna wataalamu wasiozingatia kanuni za kutoa huduma ya afya.

“Mwenye ujuzi wa kusoma vipimo na haki ya kumueleza mgonjwa ni daktari,” alisema.

Kuhusu kipimo, Stephen alisema kwa kawaida wanapopokea mkojo wa mgonjwa maabara huuotesha kwa saa 24 hadi 48 ili kutazama kama una wadudu.

“Kufanya utambuzi wa mdudu na dawa inayoweza kumuua mdudu husika nayo inaweza kuchukua saa nyingine 24. Kwa hiyo jumla inaweza kuwa saa 72 au zikaongezeka.”

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (Mat), Dk Elisha Osati alisema, “kama wapo madaktari wanaoshindwa kutafsiri vipimo kwa usahihi, sidhani kama wana sifa ya kuwa madaktari kwa sababu hakuna daktari ambaye hajasomea kutafsiri vipimo.”